Watatu wafariki, polisi akatwa mkono wakazi wakiandamana baada ya ajali Narok
MATUKIO ya kutisha yaliyonaswa kwenye video waandamanaji wakimkimbiza afisa wa polisi aliyevalia sare kamili, wakampiga na kumkata mkono yanaumiza moyo.
Inatoa taswira ya matukio ya kutishia maisha ambayo maafisa wa polisi wanakumbana nayo wakati wa kuzima maandamano nchini. Pia ilionyesha vitendo vya uhuni ambavyo vimeshuhudiwa kwa miaka mingi kati ya eneo la Ololung’a na Maai Mahiu kaunti ya Narok kwa kuziba barabara, hasa kutokana na ajali zinazohusisha mifugo.
Katika tukio la hivi punde, takriban watu watatu wanasemekana kufariki dunia kutokana na majeraha mbalimbali huku uchukuzi ukikatizwa kwenye barabara hiyo kuu kwa angalau saa 24.
Maafisa tisa wa polisi walipata majeraha tofauti huku angalau mmoja akisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu maalum katika kisa kilichotokea eneo la Duka Moja, kulingana na maafisa wa serikali.
Hii ilifuatia maandamano ya wakazi wakitaka fidia ya Sh3 milioni kufuatia kuuawa kwa kondoo 30 kwenye ajali iliyohusisha lori mnamo Alhamisi usiku.
Kamishna wa Kaunti ya Narok Kipkech Lotiatia na Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Riko Ngare walisema utulivu ulirejea eneo hilo Jumamosi, Januari 18 huku msongamano wa magari ukishuhudiwa katika barabara kuu ya Narok-Maai Mahiu kutokana na tukio hilo.
Idadi ya raia waliojeruhiwa katika ghasia hizohaikuwa imebainika kufikia wakati wa kuchapisha habari hizi huku maafisa wanane wa polisi wakitibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA