Habari za Kaunti

Watu 10 walivyoangamia ajalini Eldoret-Kitale

Na EVANS JAOLA January 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATU 10 walifariki Ijumaa, Januari 3, 2025 katika ajali ya barabarani baada ya matatu na lori kugongana karibu na kituo cha biashara cha Soi kwenye barabara kuu ya Eldoret-Kitale.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Uasin Gishu Benjamin Mwanthi alisema watoto watatu walipata majeraha mabaya na kukimbizwa katika hospitali za karibu kwa matibabu.

Ajali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya saa tatu asubuhi karibu na kituo cha biashara cha Soi wakati lori lililokuwa likisafirisha mabomba ya maji lililokuwa likielekea Kitale lilipotoka kwenye njia yake na kugonga matatu ya kampuni ya Great Rift Shuttle.

Miongoni mwa waliofariki papo hapo ni pamoja na dereva wa matatu na abiria wanane ambao bado hawajajulikana.

Abiria mwingine alitangazwa kufariki alipowasili katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi.

Bw Mwanthi alisema miili ya marehemu ilihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, ikisubiri kutambuliwa na uchunguzi wa maiti.

Dereva wa lori hilo ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo ametakiwa kujisalimisha kwa polisi.

“Tunamtaka dereva kuripoti mara moja katika kituo cha polisi kilicho karibu ili achukuliwe hatua za kisheria,” Bw Mwanthi alisema.

Magari yote mawili yaliharibiwa kwa kiasi kikubwa na kupelekwa hadi kituo cha polisi cha karibu.

Kufuatia tukio hilo, msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Dkt Resila Onyango amewataka madereva kuwa waangalifu zaidi barabarani katika msimu huu wa shughuli za usafiri baada ya sikukuu ili kuzuia ajali za barabarani kwa kuzingatia kanuni za trafiki.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA