Habari za Kaunti

Watu 15 wafariki katika ajali Bomet

Na VITALIS KIMUTAI April 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATU 15 walifariki dunia, huku wengine 11 wakijeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari matatu katika eneo la Cheptangulke, Kaunti ya Bomet, kwenye barabara ya Sotik-Kericho.

Ajali hiyo ilitokea jana alasiri baada ya magari matatu, gari la kibinafsi, matatu ya abiria 14, na lori, kugongana na kuwaua abiria kadhaa papo hapo.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, athari za ajali hiyo zilikuwa za kutisha, huku magari hayo yakibaki magofu na baadhi ya miili ya marehemu ikihitajika kutolewa kwa kutumia vifaa maalum vya uokoaji.

Maafisa wa polisi wa trafiki na timu ya uokoaji kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya waliwasili eneo la tukio kwa haraka na kusaidia kuwaokoa majeruhi kutoka kwenye mabaki ya magari.Gavana wa Bomet, Hillary Barchok, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Kaplong Mission, kwa matibabu.

“Tumehuzunishwa sana na ajali hii ya kusikitisha ambayo imegharimu maisha ya watu wengi ghafla. Tunatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na tunawaombea walioumia wapate nafuu haraka,” alisema Gavana Barchok.

Maafisa wa trafiki wanafanya uchunguzi kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, ingawa mashahidi walisema huenda kasi ya magari na kutofuata sheria za barabarani vilichangia.

Ajali hii inajiri wakati taifa linakumbwa na ongezeko la visa vya ajali za barabarani, huku wadau wa usalama wakitoa wito kwa madereva kuwa waangalifu.