Habari za Kaunti

Watu 13 wafariki katika ajali Migaa kwenye barabara ya Nakuru Eldoret

Na  JOHN NJOROGE March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATU 13—wanaume 8, wanawake 4, na mtoto mmoja—wamefariki katika ajali mbaya iliyotokea saa nane usiku katika eneo la hatari la Migaa kwenye barabara ya Eldoret-Nakuru, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Molo, Timothy Odingo, amethibitisha.

Gari la abiria la kampuni ya Kitale Shuttle lenye uwezo wa kubeba watu 11 lilikuwa likielekea Nairobi lilipogongwa kutoka nyuma na lori lililokuwa likielekea upande huo huo.

Eneo la Migaa limekuwa likijulikana kama moja ya sehemu hatari zaidi katika barabara ya Eldoret-Nakuru kutokana na idadi kubwa ya ajali mbaya zinazotokea hapo. Barabara hiyo imekuwa ikishuhudia ajali nyingi zinazosababishwa  na mwendo wa kasi wa magari makubwa, na uchovu wa madereva wanaosafiri safari ndefu.

Katika miaka ya nyuma, ajali mbaya kadhaa zimeripotiwa katika eneo hili, ikiwemo ajali ya Desemba 2017 ambapo watu 36 walipoteza maisha baada ya basi la abiria kugongana na lori.

Licha ya juhudi za serikali na wadau wa usalama barabarani, Migaa bado inaendelea kuwa eneo lenye visa vingi vya ajali, na mamlaka zinaendelea kushinikizwa kuchukua hatua madhubuti kupunguza hatari kwa watumiaji wa barabara hiyo.