Habari za Kaunti

Watu 33 wa kijiji kimoja walazwa hospitalini baada ya kula mzonga wa ng’ombe

Na  WYCLIFFE NYABERI   September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Watu 33 kutoka kijiji cha Nyakeore, eneobunge la Mugirango Magharibi kaunti ya Nyamira wamelazwa hospitalini baada ya kula nyama ya ng’ombe aliyekufa.

Mnamo Alhamisi, maafisa wa Afya ya Umma Nyamira waliarifiwa kwamba wakazi wengi wa kijiji hicho walikuwa wakiharisha sana huku wengine wakilalamikia kuumwa na tumbo.

Timu ya maafisa wa afya kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nyamira, ilitumwa mara moja hadi kijiji hicho kufanya thathmini ya kiini cha mafadhaiko yao.

Ilibainika kuwa wengi wa wale waliokuwa wakilalamikia maumivu ya tumbo walikua wameila nyama ya ng’ombe wa jirani aliyekufa siku chache zilizopita.

Uchunguzi wa sampuli zao ulionyesha uwezekano wa sumu katika nyama hiyo waliyoila kulingana na habari iliyotolewa na Idara ya Afya ya Kaunti ya Nyamira.

“Idara ya Afya ya Kaunti ya Nyamira imeripoti visa vya sumu kali ya chakula katika Kijiji cha Nyakeore, Kaunti Ndogo ya Nyamira Kusini, baada ya watu 33 kula nyama ya ng’ombe. Timu ya uchunguzi ya kaunti ilipopokea habari hiyo, ilitembelea kijiji hicho, na kuwahamisha watu hao 33 hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira. Wametibiwa na Hali Yao kudhibitiwa,” ulisema sehemu ya taarifa ya serikali ya kaunti

Kikosi cha wataala mbalimbali kimeratibiwa kutembelea kijiji hicho baadaye hii leo kufanya vipimo Zaidi na kuwasaka waathiriwa wengine.

Kufuatia tukio hilo, wakazi wa Nyamira wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa juu ya nyama ambavyo haijakaguliwa na wakati huo huo kuombwa kuzingatia viwango vya juu vya usafi ili kuepuka majanga.