Watu sita wamefariki katika ajali za mashua baharini 2024
JUMLA ya vifo sita vinavyohusiana na ajali za baharini vilirekodiwa kaunti ya Lamu mwaka huu, 2024.
Vifo hivyo vilifuatia ajali 17 za baharini zilizoripotiwa kati ya Januari na Novemba mwaka huu.
Visa hivyo vilihusisha boti na mashua kuzama baharini baada ya kusombwa na mawimbi makali, vyombo vya baharini kulipuka na kushika moto au kupasuka katikati na kuzama vikiwa katikati ya bahari, kufeli kuogelea kwa baadhi ya watu wakijivinjari baharini, vyombo kupotea na kisha mabaharia kupatikana wamekufa maji kwenye Bahari Hindi Lamu.
Kuna visa ambapo mashua na boti ziliripotiwa kutoweka baharini, ambapo shughuli za kusaka vyombo na mabaharia hao ziliendelezwa hadi kusitishwa baada ya wahusika kukosekana.
Katika mahojiano na Taifa Dijitali, Mkurugenzi wa Idara ya Majanga na Uokoaji wa Dharura, Kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi, alikiri kupungua kwa idadi ya majanga ya baharini yaliyorekodiwa 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Aidha idadi ya vifo vya baharini viliongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana, 2023.
“Mwaka huu tulirekodi visa 17 vya majanga ya baharini ambapo juhudi zilifanywa na wahusika kuokolewa. Ila tulipoteza watu 6. Mwaka jana, 2023, tulirekodi visa 22 vilivyoripotiwa, ambapo waliofariki ni 5, wengine wakiokolewa,” akasema Bw Kupi.
Kwa mujibu wa kitengo hicho cha idara ya majanga ya baharini, dhoruba kali ilishuhudiwa mwaka 2023 kwenye Bahari Hindi ilhali mwaka 2024 kukishuhudiwa utulivu wa hali ya juu, hivyo kuongeza usalama kwa wasafiri wa majini.