• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Watu watatu waangamia katika mkasa wa moto South B

Watu watatu waangamia katika mkasa wa moto South B

NA SAMMY KIMATU

WATU watatu walifariki katika kisa cha moto uliotokea Jumapili ambapo waliteketea kiasi cha kutotambulika kwa njia ya kawaida.

Naibu Kamanda wa polisi Kaunti ndogo ya Makadara Dennis Omuko alisema kisa hicho kilitokea katika nyumba moja iliyoko mkabala na barabara ya Mpweke Road katika kituo cha kibiashara cha South B, Kaunti ndogo ya Starehe.

“Waliofariki walitambuliwa kuwa ni Jackline Mutongai,35, Tamaira Karimi,4, na mwanamke kwa jina moja tu Kinya, 25,” Bw Omuko akasema.

Aliongeza kwamba miili ya watatu hao ilichukuliwa na polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi miili cha City.

Bw Omuko aliongeza kwamba maafisa wa kitengo cha upelelezi wa uhalifu wa jinai wako mbioni kuchunguza kisa hicho ili kubaini kilichosababisha mkasa huo.

Vilevile, alisema moto huo ulianza mwendo wa saa kumi na nusu usiku hadi saa kumi na moja na nusu za asubuhi.

Malori mawili ya zimamoto kutoka Serikali ya Kaunti ya Nairobi yalitumika kupambana na moto huo.

Jirani mmoja katika eneo hilo aliambia Taifa Leo kwamba walitaka kung’oa mlango wa nyumba ya wahanga lakini ulikuwa wa chuma na ulikuwa umegeuka mwekundu kwa sababu ya moto.

“Kabla ya kuangamia, tulisikia wakipiga nduru kutoka ndani ya nyumba. Tulijaribu kuvunja mlango wa chuma lakini ulikuwa moto zaidi na miale ya moto ilizuia yeyoye kukaribia,” akasema jirani huyo.

  • Tags

You can share this post!

Wanaomiliki baa wahimizwa kushirikiana na polisi kudhibiti...

Ada za juu zaanza kuwang’ata wanaosaka stakabadhi...

T L