Habari za Kaunti

Watu wawili wafariki, 50 waugua baada ya kula mlo kanisani

Na VICTOR RABALLA December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATU  wawili wamefariki kutokana na kisa kinachoshukiwa kuwa cha kula mlo uliokuwa na sumu huku wengine zaidi ya 50 wakilazwa hospitalini baada ya kula wali na maharagwe katika harambee iliyofanyika katika Kanisa la Paradiso PAG lililoko Luanda, Kaunti ya Vihiga.

Afisa Msimamizi wa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Emuhaya Dkt Martin Milimu alisema wawili hao walikimbizwa katika hospitali hiyo wakiwa katika hali mbaya na walifariki walipofika katika kituo hicho.

Alisema wagonjwa hao wanashukiwa kutumia chakula chenye sumu siku ya Jumapili na walitafuta matibabu katika hospitali hiyo Jumatatu.

Walitafuta matibabu

“Kwa sasa tuna watu 56 waliolazwa wakiwa na dalili za kutapika na kuharisha lakini kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri,” alisema.

Alifichua kuwa sampuli  zimepelekwa katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (Kemri) na Huduma ya Kitaifa ya Maabara ya Afya ya Umma jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi.

Dkt Milimu ambaye aliandamana na Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Vihiga Dkt Mary Susan Anyienda alisema timu ya wachunguzi wa magonjwa katika kaunti hiyo ilifanikiwa kudhibiti hali iliporipotiwa kuzuka.

Walioathiriwa ni pamoja na waumini kutoka makanisa 10 katika Kaunti Ndogo za Luanda na Emuhaya.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa makanisa hayo Mchungaji Kennedy Kimiya, tukio hilo lilitokea baada ya waumini hao kula chakula kilichoandaliwa na mmoja wa wazee wa kanisa hilo.

“Inatia shaka kwamba aliandaa mlo huo Jumamosi usiku  kuwahudumia  watu waliojitokeza kushiriki katika harambee ya kusaidia ujenzi wa kanisa hilo,” alisema.

Walibeba chakula kupatia familia zao

“Baadhi ya wanachama walibeba chakula hicho nyumbani na kupatia familia zao,” alisema Bw Kimiya na kuongeza kuwa watu sita wa familia moja waliathirika na kulazwa katika hospitali ya Emuhaya.

Mapasta watano wa PAG pia wamelazwa baada ya kula chakula hicho chenye sumu.

Mchungaji Patrick Watate alisema mshukiwa alikamatwa na anachunguzwa na Maafisa wa Upelelezi wa Jinai.

Dkt Anyienda  alitoa wito kwa wale wote wanaoonyesha dalili zinazonana na hali hiyo  kutafuta matibabu haraka iwezekanavyo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA