Habari za Kaunti

Wauguzi, wahudumu wa matibabu waanza mgomo Uasin Gishu

Na TITUS OMINDE December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKAAZI wa Kaunti ya Uasin Gishu wanaosaka huduma za kimatibabu msimu huu wa Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya watahangaika baada ya wauguzi kugoma.

Wauguzi 500 na wahudumu wengine wa huduma za afya walianza mgomo wao Jumatatu, Desemba 23, 2024.

Mgomo huo ulianza baada ya makataa ya ilani ya mgomo husika iliyotolewa Desemba 10.

Wauguzi waliogoma wakiongozwa na katibu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi Kenya (KNUN), Tawi la Uasin Gishu, Kleen Kimutai walisema uamuzi wa kuanzisha mgomo uliafikiwa baada ya kaunti kushindwa kushughulikia maslahi ya wauguzi.

Akizindua mgomo huo katika uwanja wa Kipchoge Kipkeino, Bw Kimutai alitangaza kusitishwa rasmi kwa huduma za afya katika vituo vyote vya afya katika kaunti hiyo.

Bw Kimutai alishutumu uongozi wa kaunti kwa kuwakatisha tamaa wauguzi waliotoa malalamishi yao kwa wakati jinsi ilivyoainishwa katika sheria ya viwanda.

Miongoni mwa masuala ambayo yamesababisha mgomo huo ni pamoja na kucheleweshwa kupandisha vyeo wauguzi, licha ya mazungumzo kadhaa na kaunti kushughulikia suala hilo.

Maafisa hao wa KNUN walisema licha ya mawasiliano ya mara kwa mara na mwaajiri, kutuma barua na kutafuta mikutano, juhudi zao za kutatua utata huo zimeambulia patupu.

“Licha ya majaribio yetu mengi ya kushirikisha utawala wa kaunti kwa nia njema, ikiwa ni pamoja na kuandika barua na kutafuta mazungumzo rasmi na bodi, tumepuuzwa,” alisema Bw Kimutai.

Bw Kimutai alisema tabia ya kupuuza wauguzi wengi katika kaunti hiyo imechangia kuzorota kwa huduma za afya.

Alisema kuwa uamuzi wa kuanza mgomo ulisababishwa na kuendelea kwa serikali ya kaunti kutojali maslahi ya wauguzi.

Alikashifu kaunti kwa kukosa kuheshimu ahadi za awali zilizotolewa kwa chama cha wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa kupandishwa vyeo kwa muda mrefu, kuteuliwa upya kwa wauguzi waliobobea, kuwasilisha kwa wakati makato ya kisheria, na kupitisha muundo wa mishahara ya 2024 uliopendekezwa na Tume ya SRC.