Habari za Kaunti

Wauzaji mitumba wakubaliwa kuishtaki serikali ya Sakaja

June 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA 222 wa kuuza nguo za mitumba katika soko la Gikomba wamekubaliwa na Mahakama Kuu kuwasilisha kesi kupinga kubomolewa kwa vibanda vyao kwenye ardhi ya ekari mbili na Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Jaji Opande Aswani aliruhusu wafanyabiashara hao kuwasilisha ushahidi wa leseni walizopewa na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuendeleza biashara hiyo.

Jaji huyo alifahamishwa kwamba mbali na leseni walizopewa kuendeleza biashara zao, pia Rais William Ruto aliwahakikishia wakati wa kampeni zake 2022 kwamba hawangefukuzwa kutoka Gikomba na wala vibanda vyao vya kuuzia nguo havingebomolewa.

“Rais Ruto aliwahakikishia wafanyabiashara hawa ambao wamehudumu katika soko hili la Gikomba kwa miaka 78 hawatafukuzwa. Alinunua shati la Sh100 kutoka Gikomba kama ishara ya kuwaunga mkono wafanyabiashara hawa,” wakili Danstan Omari alisema.

Mahakama ilisema ni heri walalamishi hao wawasilishe kesi upya ndipo wajumuishe ushahidi wote.

Korti ilielezwa matingatinga ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi yalibomoa vibanda kwenye ekari mbili zilizo na thamani ya Sh1 bilioni kupata nafasi ya kujenga egesho la magari ya zimamoto.

Lakini mahakama ilielezwa egesho hilo linafaa kujengwa kwa uwanja wa ukubwa wa mita 50 kwa mita 50 na wala sio ekari mbili.

“Ni bayana mabwanyenye wanamezea mate uwanja huu na wanasingizia suala la zimamoto kuunyakua,” mahakama ilifahamishwa.

Pia Jaji Opande alifutilia mbali agizo la hapo awali la kuwaagiza wafanyabiashara hao walipie gharama ya kesi hiyo.

Bw Omari aliomba korti iwahurumie wafanyabiashara hao ambao wamelipia leseni za biashara zao kwa kaunti na huku korti ikiwabebesha mzigo wa kulipia gharama ya kesi.

Mahakama ilielezwa tayari wafanyabiashara wawili waliaga dunia baada ya vibanda vyao kubomolewa.

Jaji Opande alimpa Bw Omari saa mbili kuwasilisha kesi upya.