Wauzaji mitumba wapinga ubomoaji vibanda sokoni Gikomba
NA RICHARD MUNGUTI
WAFANYABIASHARA wawili wa kuuza nguo za mitumba wamefariki kutokana na mshtuko baada ya vibanda vyao kubomolewa katika soko la Gikomba, Jaji Opande Aswani wa Mahakama Kuu jijini Nairobi ameelezwa.
Jaji Aswani alifahamishwa na wakili Danstan Omari kwamba matingatinga ya serikali ya Kaunti ya Nairobi yanaendelea kubomoa nyumba na vibanda vya biashara katika soko hilo la wazi lililoko baina ya Pumwani na Kariokor.
Jaji huyo aliombwa asitishe ubomoaji huo hadi pale kesi iliyoshtakiwa na wakazi na wafanyabiashara 220 itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Mahakama Kuu ilielezwa kwamba walalamishi wameishi katika makazi hayo tangu mwaka wa 1932 na “kamwe hawajaonyeshwa mahala mbadala pa kuendeleza biashara zao.”
Akiomba mahakama isitishe ubomoaji huo, Bw Omari alimfahamisha Jaji Aswani kwamba soko hilo linawafaidi zaidi ya watu 5 milioni katika eneo hili la Afrika Mashariki.
“Watu wanaofaidika na soko la Gikomba na biashara hii ya uuzaji mitumba mbali na Wakenya, ni watu wa mataifa ya Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” Bw Omari alisema.
Wakili huyo alieleza mahakama kwamba wafanyabiashara hao wanatimuliwa kwa ardhi hiyo ipewe mabwanyenye watakaojenga majumba ya kuwekeza biashara iyo hiyo.
Jaji Aswani alimruhusu Bw Omari kuwasilisha kesi upya na kumruhusu wakili Dida Halake anayewakilisha serikali ya kaunti ya Nairobi siku saba kujibu masuala mapya katika kesi hiyo.
Wafanyabiashara hao wamelalamika kwamba hawakupewa notisi na kwamba wamelipa kwa kaunti ada zote zinazohitajika.
Jaji Aswani aliwaamuru mawakili Halake na Omari wawasilishe tetezi zao kufikia Juni 7, 2024, ndipo atoe uamuzi ikiwa atasitisha ubomoaji huo au la mnamo Juni 10, 2024.