Habari za Kaunti

Wavinya akemea ufisadi akibeba msalaba Ijumaa Njema ya Pasaka

March 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti ametoa changamoto kwa Wakenya kuepuka ufisadi, akiutaja uovu huo kuwa tishio kubwa kwa maendeleo na utoaji huduma.

Akihutubia waumini wa Kanisa Kikatoliki wakati wa Misa ya Pasaka katika kanisa la Mama of Lourdes Cathedral mjini Machakos, Gavana Ndeti aliwataka Wakristo kujiepusha na maovu kama njia mojawapo ya kusaidia serikali  kutoa huduma muhimu kwa umma.

“Nyote mnajua ushuru wa kaunti unapaswa kulipwa kupitia huduma ya MPESA. Lakini bado unapata watu wakifanya malipo kwa pesa taslimu. Mtoaji na mpokeaji wanafanya  makosa kwa sababu wanasaidia kuhimiza ufisadi,” alisema gavana Ndeti.

Gavana huyo alisema kwa kufanya malipo kupitia M-Pesa, Serikali ya Kaunti itakuwa katika nafasi ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Sahau kuhusu kelele za wahujumu. Nitahakikisha kwamba ushuru wenu unatumika ipasavyo. Wanaopiga kelele wamezoea kupora rasilimali za umma,” aliongeza.

Naibu Gavana, Francis Mwangangi, aliyeandamana na Bi Ndeti, aliunga mkono maoni yake, akiwataka Wakristo waepuke dhambi ya ufisadi.

Bw Mwangangi alimpongeza gavana kwa kuchaguliwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Kaunti za Kusini Mashariki mwa Kenya (SEKEB) wakati wa mkutano uliofanyika katika Kaunti ya Makueni.