Wavinya akumbana na upinzani mkali kwa mpango wa kukausha bwawa la Tala
HATUA ya utawala wa Gavana wa Machakos, Wavinya Ndeti kukausha bwawa la Tala lililodumu kwa takriban miaka 90 na kuligeuza kuwa kituo cha matatu imepingwa vikali na wakazi wa eneo hilo.
Wafanyabiashara na wakazi wanaopinga mpango wa bwawa hilo lililoko katika Kaunti-ndogo ya Matungulu wanasema hatua hiyo itasababisha uhaba mkubwa wa maji.
Badala yake, wamemtaka Bi Ndeti na utawala wake kuanza mpango wa kulisafisha bwawa hilo ambalo wanasema limechafuliwa mno.
“Tunategemea Bwawa la Tala kukabiliana na ukame kwa sababu Mji wa Tala uko katika eneo linalopata mvua chache. Bwawa hili ndilo chanzo chetu kikuu cha maji. Kwa hivyo, hakuna yeyote anayepaswa kufikiria kulikausha,” alisema James Mwovi.
Taifa Leo imebaini kuwa mpango wa kubadilisha matumizi ya Bwawa la Tala ni sehemu ya mpango mpana wa serikali ya kaunti wa kupanga upya mji huo unaokua kwa kasi katika siku za karibuni.
Meneja wa Manispaa ya Kangundo-Tala Justus Kiteng’u, pamoja na Mwakilishi wa Wadi ya Tala Jackson Ndaka, walisema mpango huo unahusisha kuhamisha kituo kikuu cha mabasi kutoka eneo la kibinafsi ambako kinapatikana kwa sasa.