Wavinya motoni MCAs wakitishia kumtimua ofisini
BAADHI ya madiwani wa Kaunti ya Machakos wametishia kumtimua Gavana wa Machakos, Wavinya Ndeti, kufuatia hatua ya wenzao wanaomuunga mkono gavana huyo ya kuanzisha mchakato wa kumng’oa Spika wa Bunge la Kaunti hiyo, Anna Kiusya, hali ambayo imeongeza joto la kisiasa katika kaunti hiyo.
Diwani wa Kinanie/Mathatani, Wambua Kavyu, na mwenzake wa Muthwani, Dominic Maitha, wameanza kampeni ya kumng’oa Bi Ndeti ofisini wakimlaumu kwa utawala mbaya.
“Kawira Mwangaza sasa yuko nyumbani baada ya kudharau madiwani wa Meru. Wewe sio spesheli. Bado sijachelewa kuwasilisha hoja ya kumuondoa Bi Ndeti kwa sababu hashughulikii utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Bw Maitha kwenye mkutano wa hadhara Jumanne.’
“Kama wakazi wa Muthwani na Joska, hatuna cha kuonyesha licha ya mabilioni ya shilingi ambazo Machakos hukusanya kupitia kodi kila mwaka. Bi Ndeti anawadharau madiwani, na kwa sababu hiyo lazima aondoke,” aliongeza diwani huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM.
Taifa Jumapili linafahamu kuwa mpango wa kumtimua Bi Ndeti unachochewa na juhudi za baadhi madiwani wanaomuunga mkono Gavana huyo kuanzisha hoja ya kumuondoa Bi Kiusya.Jumla ya wawakilishi wadi 33 kati ya 59 walitia saini hoja ya kumwondoa Bi Kiusya katika mkutano uliofanyika hoteli moja jijini Nairobi siku ya Jumatatu.
Hoja hiyo inatarajiwa kuwasilishwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Machakos, Nicholas Nzioka, pindi madiwani watakaporejea kutoka mapumzikoni.
Kulingana na notisi ya hoja iliyopokelewa na Bunge la Kaunti Jumatano, sehemu ya madiwani wakiongozwa na Bw Nzioka, wamesema kuwa Bi Kiusya anakabiliwa na mashtaka manane, yakiwemo ufisadi na uzembe kazini.
“Bi Kiusya alihusika katika kuajiri mtu anayemfahamu vyema ndani ya Bunge la Kaunti bila kufuata taratibu zinazostahili. Nafasi hiyo haikutangazwa hadharani, jambo ambalo linakiuka Kifungu cha 232 cha Katiba kinachohakikisha ushindani wa haki na uteuzi wa umma kwa misingi ya sifa,”alisema Bw Nzioka katika moja ya mashtaka hayo.
Aidha, anamtuhumu Bi Kiusya kwa kutumia vibaya fedha za umma kugharamia safari ya binti yake kwenda Ufalme wa Kiarabu na Uingereza mwaka wa 2023 bila sababu za msingi.Jaribio la Taifa Jumapili kuwasiliana na Bi Kiusya kwa simu halikufua dafu.
Hata hivyo, madiwani wanaompinga Bi Ndeti walijitokeza haraka kumtetea Bi Kiusya, wakidai kuwa mpango wa kumtimua ni jaribio la Gavana kumtisha Spika huyo.