• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Wavuvi wanne wajeruhiwa kwa mlipuko wa mashua

Wavuvi wanne wajeruhiwa kwa mlipuko wa mashua

NA KALUME KAZUNGU

WAVUVI wanne wamejeruhiwa vibaya baada ya mashua walimokuwa wakisafiria kuteketea eneo la Ras Kiamboni kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.

Wavuvi hao Wakenya walikuwa wakisafiri kutoka Somalia kuingia Lamu baada ya kuenda nchi hiyo jirani kununua shehena za samaki.

Afisa wa Kitengo cha Majanga ya Dharura katika Kaunti ya Lamu Bw Shee Kupi amethibitisha ajali hiyo mnamo Ijumaa, akitaja kuwa ajali hiyo ya moto mashuani ilisababishwa na petroli iliyokuwa ikivuja kwenye mtungi mmoja uliobebwa chomboni.

Bw Kupi aliwashukuru wanajeshi (KDF) kwa juhudi zao katika kuokoa maisha ya wavuvi hao walioungua mikono, miguu, mabega na pia vifuani.

Waliojeruhiwa walikimbizwa na KDF hadi kwenye kambi yao ya Ras Kiamboni, ambapo walipokezwa huduma ya kwanza kabla ya kusafirishwa kwenye hospitali kuu ya rufaa ya King Fahd iliyoko Lamu wanakoendelea kupokea matibabu.

“Kuna wavuvi wanne ambao wamenusurika kifo mashua yao ilipolipuka na kuungua baharini eneo la Ras Kiamboni, mpakani mwa Kenya na Somalia. Ni wavuvi wa Lamu. Twashukuru KDF kwa jitihada zao zilizosaidia kuokoa maisha ya wavuvi wetu,” akasema Bw Kupi.

Si mara ya kwanza kwa mashua kulipuka na kuungua na hata kujeruhi mabaharia Lamu.

Mnamo Februar 2020, mtu mmoja alijeruhiwa vibaya pale boti lilipolipuka na kuungua vibaya kisiwani Lamu.

Boti hilo ambalo injini yake hutumia petroli linaaminika kuchomeka kwa moto uliochangiwa na kuwashwa kwa sigara na jamaa huyo aliyejeruhiwa kwa kuunguzwa na moto huo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume atupwa rumande kwa kushindwa kulipa bili hotelini

Kalonzo aungana na Mawakili kumwambia Ruto aheshimu mahakama

T L