Habari za Kaunti

Wazee kumbembeleza Arati akubali mazungumzo ya kuzima uadui na Osoro

January 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

WANASIASA wakongwe na wazee wengine kutoka jamii ya Abagusii, wameahidi kumbembeleza Gavana wa Kisii Simba Arati akubali kuhudhuria vikao vya maridhiano, vinavyolenga kumpatanisha na hasidi wake wa kisiasa, mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro.

Kufuatia ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika gatuzi hilo siku za hivi karibuni, ambazo zimeanza kuhatarisha maisha ya wakazi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alianzisha juhudi za kuleta uwiano baina ya wawili hao.

Lakini gavana Arati alidokeza kwamba hatahudhuria vikao hivyo, akishikilia kwamba Bw Osoro ndiye amekuwa akimchokoza na hivyo aliitaka serikali imkamate mbunge huyo wa UDA, ambaye pia ni Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Isitoshe, gavana Arati alidai kuwa Bw Machogu ana mkono fiche katika ‘kuhangaishwa’ kwake na akaongeza kuwa waziri huyo hatakuwa mpatanishi mzuri.

Licha ya pingamizi hiyo kutoka kwa Bw Arati, vikao vya kwanza vya patanisho vilifanyika jijini Nairobi mnamo Januari 17, 2024, kama ilivyokuwa imepangwa.

Aliyekuwa seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri na mbunge wa zamani Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi walikuwa miongoni mwa watu tajika waliohudhuria mkutano huo. Bwc Arati hata hivyo alisusia mkutano huo alivyoapa lakini Bw Osoro alikuwepo.

Baada ya kushiriki mazungumzo kwa muda wa saa kadhaa, kamati hiyo ya maridhiano iliamrisha kuwe na kusitishwa kwa makabiliano baina ya viongozi hao wawili.

Katika taarifa iliyotolewa na wapatanishi hao, walisema ilikuwa muhimu kwa viongozi wote katika sekta zote kukutana kwa dhamira ya kuhakikisha amani inapatikana Kisii.

“Baraza la wazee limejadili kwa kirefu juu ya njia zinazowezekana za kusuluhisha masuala yote na kurejesha amani na maelewano Kisii. Tunatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano ya kisiasa. Baraza la ushauri la Wazee wa Kisii litajadili zaidi masuala mengine yote yanayoathiri jamii. Wazee wa Gusii watazungumza na gavana Simba Arati, na Mbunge wa Mugirango KusiniĀ  Sylvanus Osoro kuhusu jinsi ya kuweka, na kudumisha, amani katika gatuzi letu,” ilisoma sehemu ya taarifa ya wazee hao.

Wazee hao pia waliongeza kuwa watazidi kufanya vikao na viongozi wote waliochaguliwa kwa kuwahusisha viongozi wa makanisa.

Waliviomba vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ambayo yamejiri Kisii na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya waanzilishi wa ghasia hizo bila kujali nyadhifa zao katika jamii.

Mlezi wa sasa wa Baraza la Wazee wa Abagusii Steve Omenge Mainda, alichaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Ushauri wa patanisho hiyo.