Habari za Kaunti

Wenye matrela waonywa baada ya kontena ya mizigo kuangukia matatu njiani

Na MISHI GONGO August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ABIRIA watano walijeruhiwa vibaya huku wengine wanane wakipata majeraha madogo baada ya kontena ya mizigo kupinduka na kuangukia matatu ya abiria 14 kutoka kwa trela katika eneo la Kibarani, Kaunti ya Mombasa, Jumamosi usiku.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Changamwe, Bw Edward Muchama, alisema waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Coast General ambapo wanapokea matibabu.

“Wale watano waliopata majeraha mabaya wako katika hali dhabiti, huku wengine wakitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani. Tunaendelea kufuatilia hali yao kwa karibu,” alisema Bw Muchama.

Kwa mujibu wa ripoti za polisi, kontena hiyo, ambalo lilikuwa tupu wakati wa ajali, liliachika kutoka kwa trela na kuangukia matatu iliyokuwa ikisafirisha abiria kuelekea mjini.

Afisa huyo aliwataka madereva wa malori kuhakikisha kontena zimefungwa vyema ili kuepusha ajali kama hizo siku zijazo.

“Tunaomba madereva na wasafirishaji wakague mizigo yao mara mbili. Uzembe wa aina hii unaweka maisha ya watumiaji barabara wasio na hatia hatarini,” alisema Bw Muchama.

Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye Barabara Kuu ya Mombasa–Nairobi huku vikosi vya uokoaji vikishirikiana na polisi na wakazi kufungua njia.