Habari za Kaunti

Wito kina mama wafuatilie wasichana wasipachikwe mimba

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA OSBORN MANYENGO

WITO umetolewa kwa kina mama katika Kaunti ya Trans Nzoia kuwachunga watoto wao wasichana kuzuia visa vya mimba za mapema.

Kamishna wa Kaunti Trans-Nzoia Bw Gideon Oyagi alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Sikhendu wakati wa hafla ya upanzi wa miti eneo la Weonia, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Bw Oyagi alisema visa vya mimba za mapema vimeaongezeka sana, akidai vinatokana na kina mama kutuwajibikia malezi ya mtoto msichana.

Bw Oyagi alisema ni jukumu la mama mzazi au mlezi kufuatilia mienendo ya mtoto wa kike kwa kujua ni wapi anaenda.

Alisema kina mama wengi huwaacha watoto wao wa kike kwenda kurandaranda huku na kule.

Pia aliwaonya kina mama dhidi ya kuacha mtoto wa kike na baba yao ndoa inaposambaratika.

“Kuna wanaume wengine ni wanyama… huwezi ukamuachia mtoto wa kike ndoa inaposambaratika. Pia utapata mama anamuamini mtu wa kiume hata kama ni jirani ama wa ukoo anamuweka karibu na mtoto wa kike… chungeni sana nyinyi kina mama,” akasema Bw Oyagi.

Kamishna huyo alitoa wito kwa maafisa wa utawala, chifu, na manaibu wa chifu kushirikiana na wazee wa Nyumba Kumi kuona kwamba hakuna mtoto anapatikana nyumbani bila sababu ya kutoenda shuleni.

Alisema elimu kwa shule za upili za kutwa ni bura ambapo serikali inalipia mwanafunzi pesa kiasi fulani, akionya wale ambao wamezoa kutuma mtoto ambaye anafaa kuwa shule, kwenda kutafuta pesa.