Habari za Kaunti

Yafichuka kaunti hutuma makarani kufunza watoto wa chekechea

September 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Nyandarua imemulikwa baada ya kufichuka kwamba imekuwa ikitumia makarani kuwafunza watoto wachanga katika shule za chekechea.

Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Elimu katika kikao, Jumanne, ilibaini kwamba jumla ya maafisa 178 walioorodheshwa na Bodi ya Kuajiri Wafanyakazi wa Kaunti (CPSB) kama makarani, wanatumika kuwafunza watoto wa PP1 na PP2 kaunti hiyo.

Gavana Moses Kiarie alikabiliwa na wakati mgumu kufafanua sababu ya kuwatumia makarani kufanya kazi ya ualimu bila stakabadhi zinazohitajika kufunza shule za chekechea wala kusajiliwa na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC).

“Hawa ni makarani. Kuna tofauti kati ya karani na mwalimu. Kwa nini unaruhusu karani kufunza bila kufuzu kielimu?” aliuliza Seneta Seki ole Kanar (Kajiado).

“Ingeeleweka kama ni wafanyakazi wasaidizi lakini sio karani. Hawawezi kuwa na nambari za TSC kwa sababu si wataalam.”

Akijitetea, Gavana Kiarie alieleza Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta Mteule Betty Montet kwamba wafanyakazi hao, wengi wao wanaoelekea kustaafu, walirithiwa kutoka serikali ya manispaa iliyovunjiliwa mbali.

Kamati hiyo ilielezwa maafisa hao walioorodheshwa katika daraja F sawia na makarani, walitumwa kufunza katika shule za chekechea kwa sababu hawakufuzu kuwa katika idara nyingine yoyote.

“Viwango vyao vya kufuzu havingetoshea popote katika sera ya taaluma na hatungewafuta kazi. Hawajaorodheshwa popote na tunatumia daraja hilo kuwalipa. Tunawachukulia kama wafanyakazi wasaidizi 1 na 2,” alifafanua Gavana.

Kulingana naye, maafisa hao ni “watu ambao wamefunza Nyandarua kwa miaka 20 -30 na hata wanafanya kazi bora zaidi”.

Hata hivyo, wanakamati wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti Prof Margaret Kamar, walitilia shaka ufafanuzi wa Gavana hasa kuhusiana na idadi ya wafanyakazi waliohamishwa kutoka baraza la manispaa. Seneta John Nderitu (Laikipia) alitaja idadi hiyo kuwa ya “kuhofisha” akisema “haiwezekani kwamba kaunti ilirithi makarani 178.”

Profesa Kamar alielezea wasiwasi kuhusu hatma ya watoto wachanga katika Kaunti ya Nyandarua akimshutumu Gavana kwa kudunisha elimu ya chekechea aliyotaja kuwa muhimu zaidi.

“Unaua elimu ya mtoto wa chekechea. Yamkini huoni umuhimu wa PP1 na PP2,” alihoji.

“Usipomkuza mtoto na elimu inayofaa haukuzi chochote. Ninahofia kwamba unatumia makarani kwenda kufundisha shule za chekechea na si haki kamwe.”

Seneta Kamar aliilaumu bodi ya kuajiri wafanyakazi Nyandarua kwa kuruhusu makarani walioajiriwa kwa kandarasi ya kudumu kutumika kama walimu bila kufuzu.

“Makarani ni wengi kuliko walimu. Mbona uliwapa ajira ya kudumu bila hata mafunzo ya kuwageuza kuwa walimu. Basi tuna tatizo,” alisema.