Zaidi ya maskwota 1,200 eneo la Kisauni kufurushwa
NA BRIAN OCHARO
ZAIDI ya maskwota 1,200 wanaoishi kwenye kipande cha ardhi cha ekari 341 huko Kisauni huenda wakafurushwa katika eneo hilo baada ya Mahakama ya Mombasa kukataa kumplipa mwenye ardhi hiyo fidia ya Sh1.7 bilioni ili kuwaruhusu maskwota hao kuendelea kuishi kwenye ardhi hiyo.
Badala yake, Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Stephen Kibunja ametoa muda wa siku 60 kwa mashirika husika serikalini na maskwota kushirikiana na uongozi wa Kampuni ya Mainland Properties Ltd kutafuta suluhu ya kudumu.
“Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Waziri wa Ardhi Alice Wahome na Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome wamepewa siku 60 kuzungumza na pande zote husika na kutafuta suluhu ya makazi mapya kwa maskwota hao,” alisema Jaji Kibunja.
Jaji huyo pia alibaini kuwa amri ya mahakama iliyotolewa Februari 2017 ya kuwafurusha maskwota hao itatumika ikiwa hakuna suluhu itakayofikiwa ndani ya muda uliowekwa.
Kampuni hiyo ilielekea mahakamani mwaka wa 2018 kuomba amri mbalimbali, zikiwemo usaidizi wa polisi katika kuwaondoa wavamizi hao na pia kulipwa fidia ya jumla kwa ukiukaji wa haki zake za kumiliki na kufurahia mali yake.
Zaidi ya hayo, kampuni hiyo ilitaka kulipwa fidia maalum kwa kupata hasara ya kutotumia ardhi hiyo kutoka Oktoba 1984 hadi Julai 2017.
Pia, iliomba fidia ya Sh28.2 milioni kama gharama zilizotumika katika kuunda ramani za mapendekezo ya maendeleo, wahandisi, washauri na ada za wabunifu kwa ajili ya mradi wake wenye thamani ya Sh5 bilioni.
Kupitia Karim Anjarwalla, kampuni hiyo ilisema imepata hasara kwani haikuweza kuendelea na mradi wa uendelezaji katika ardhi hiyo kutokana na kuvamiwa na maskwota.
Watu wasiopungua 3,438 walikuwa wameomba kujiunga na kesi hiyo, lakini ni maskwota 1,219 pekee waliokubaliwa kuingia kama Kajiweni Asili CBO.
Pia, waliwasilisha ombi lao tofauti na kudai haki za umiliki wa ardhi hiyo. Kampuni hiyo ilisema kuwa Plot No. 828/ II/ MN imesajiliwa kwa jina lake tangu Desemba 1982.
Mlalamishi huyo alidai kuwa eneo hilo liliponunuliwa, kulikuwa na familia sita zilizoishi hapo, lakini kufikia 2001, idadi hiyo iliongezeka hadi 69 ma kuwa idadi hiyo iliongezeka hadi maelfu ya watu kufikia sasa.
Kampuni hiyo ilisema juhudi za kuwaondoa maskwota hao kwenye ardhi yake imeambulia patupu tangu wakati huo.
Serikali kupitia kwa Bw Barnabas Ng’eno iliwasilisha ombi la dharura likiomba amri ya kutupilia mbali kesi ya kampuni hiyo ikisema inatafuta njia ya kujipatia mali.
Pia, serikali lilidai kuwa lilijaribu kutekeleza maagizo ya kuwafurusha maskwota hao lakini juhudi hizo hazikufaulu kutokana na maafisa wa polisi kujeruhiwa na maskwota hao.
“Takriban maafisa 50 wa polisi waliotumwa kutekeleza agizo la mahakama kwenye ardhi inayozozaniwa hawakuweza kufaulu na wakaishia kupata majeraha,” serikali iliripoti.
Jaji huyo alikiri kuwa kampuni hiyo ya kibinafsi ilidhihirisha umiliki wake wa ardhi hiyo.
Pia, jaji Kibunja alizingatia pendekezo la fidia kama suluhu linalofaa kwa suala la makazi mapya ya maskwota, na kuhakikisha kuwa mlalamishi, kama mmiliki wa mali, anafidiwa kwa haki ili ardhi ichukuliwe.
“Hata hivyo, kwa kuwa hakuna ushahidi kwamba serikali imemshirikisha mlalamishi juu ya pendekezo hilo au kupata maelewano yake, mahakama haitazingatia kutoa aina hiyo ya amri,” alisema Jaji.
Jaji Kibunja, hata hivyo alibaini kuwa pande zote zinafaa kuwa huru kutekeleza wazo hilo na ikiwezekana kuleta Tume ya Kitaifa ya Ardhi na Serikali ya Kaunti husika ili kuona ikiwa azimio lililokubaliwa kuhusu pendekezo hilo linaweza kufanikiwa.