Habari za Kitaifa

Abiria walilalamikia ubovu wa basi safari nzima kabla ajali ya kutisha

Na JOHN NJOROGE August 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BASI lililohusika katika ajali iliyoua watu 14 Jumanne asubuhi katika eneo la Migaa kwenye barabara ya Nakuru- Eldoret lilikuwa limepata hitilafu mara kadhaa safarini, manusura wanasema.

Basi hilo la kampuni ya Coast Bus lilikuwa likielekea Mombasa kutoka magharibi mwa Kenya, ajali hiyo ilipotokea mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

Mkuu wa polisi eneo la Molo, Bw Tom Odingo, alisema watu 13 walifariki katika ajali iliyohusisha magari kadhaa.

Kamanda wa polisi eneo la Rift Valley, Bw Jaspa Ombati, alisema waliofariki ni wanawake watano, wanaume saba na mtoto mchanga.

Mmoja wa manusura, Bi Rhoda Atieno, aliambia Taifa Leo kwamba kabla ya ajali, basi hilo la kubeba abiria 60, lilikuwa limepata matatizo katika safari.

Mabaki ya basi la kampuni ya Coast Bus lililohusika katika ajali ya barabarani eneo la Migaa, karibu na Salgaa. Picha|John Njoroge

“Abiria walikuwa wakilalamika hasa katika maeneo ya milima. Nilisikia sauti baada ya dereva kupiga kamsa akisema breki zilikuwa zimefeli kabla ya kugonga gari la kibinafsi,” alieleza.

Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, lilifichua kuwa takriban watu 55 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea karibu na eneo la Salgaa.

“Watu 36 waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali za Molo na Coptic kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na magari mengi eneo la Migaa huko Molo, Kaunti ya Nakuru,” Shirika la Msalaba Mwekundu likasema.

Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali za Coptic na Molo kwa matibabu huku waliofariki wakipelekwa katika mochari za hospitali hizo hizo.

Wakati huo huo, polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.