Abiria wamechoka: Bodaboda wasiooga wamulikwa
WAHUDUMU wa bodaboda eneo la Mlima Kenya wamezindua msako wakilenga wenzao ambao wamegomea maji msimu huu wa kijibaridi kikali kinachotokana na mvua ya maangamizi.
Hii ni baada ya malalamishi kutolewa kwamba baadhi ya wahudumu wa bodaboda hunuka kama panya aliyeoza.
Abiria ambao ni kawaida katika uchukuzi wa aina hiyo kukaa karibu na waendeshaji bodaboda, wanalazimika kuvumilia uvundo huo, huku wakifufinika mianzi ya pua.
Mwenyekiti wa Muungano wa Masilahi ya Wanabodaboda na Tuk Tuk (BR&RSWA) Bw Daniel Kariuki, aliambia Taifa Leo mnamo Jumanne kwamba amepokea malalanishi mengi kuhusu bodaboda wachafu.
“Tumeambiwa kwamba baadhi ya bodaboda wenzetu wamekataa kuoga. Sanasana wengi ambao wamekataa usafi ni wale ambao hawajaoa, walevi na watumizi wa mihadarati,” akasema Bw Kariuki.
Bw Kariuki alisema kwamba kwa kawaida wanabodaboda wengi huvalia nguo nyingi kwa mpigo kujikinga na athari za upepo na hivyo basi kuwafanya waogope kuzitoa ili waoge.
Wengine wamekuwa wakitelekeza usafi wa kimsingi kutokana tu na wao kujisahau na kuchukulia usafi wa mwanamume kimzaha.
Akiongea mjini Nyeri, alisema kwamba kukiri kwake kwamba muungano wao una wanachama ambao hawaogi hakulengi kuwakejeli au kuwaaibisha.
“Ni ukweli ambao hata tukiuficha, wateja wanajua uko,” akasema Bw Kariuki.
Alisema kwamba ni lazima kwa bodaboda yeyote awaye kujizatiti kujikomboa kutokana na nembo mbovu ya uchafu.
Aliagiza kwamba ni lazima kwa bodaboda kuangaliana na wote ambao hawaogi na wanajitokeza kazini wakinuka kama mayai viza, basi watimuliwe stejini.
Hata hivyo, Bw Kariuki alisema kwamba “sijapigia debe visa vya kuwasakama wetu wachafu na kuwaosha hadharani kwa kuwa hilo ni kinyume na sheria”.
Alisema kwamba haki za kibinadamu haziruhusu yeyote kumvua nguo mwenzake na kumuosha kimabavu kwa kuwa hilo ni sawa na kutekeleza uvamizi wa kudunisha na kuaibisha.
“Hata hivyo, wachafu miongoni mwetu wanaweza wakachukuliwa na rika lao, wapelekwe kwa vyoo na mabafu ya umma mjini, walipiwe ada na hatimaye nje ya bafu husika, kushikwe doria ndipo ithibitishwe kwamba walengwa hao wanaoga,” akasema.