Habari za Kitaifa

Achani ahimiza wabunge kuunda sheria ya kupiga marufuku muguka

June 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kwale Fatuma Achani amewataka wabunge kutoka Kwale kwenda katika Bunge la Kitaifa na kubuni sheria ya kupiga marufuku biashara ya muguka.

Bi Achani alisema kisheria, kaunti hazina ruhusa ya kupiga marufuku biashara ya muguka.

Alisema ameokoa fedha za umma kwa kutopiga marufuku mmea huo ambao umehalalishwa na serikali kuu.

“Mimi ni wakili, nilipoangalia swala lote zima la muguka nikaona nikipiga marufuku haitofanya kazi sababu sheria iliyopo nchini kuhusu mmea huu inaunga mkono muguka. Ningepiga marufuku ningepelekwa kortini na kuna gharama yake ikiwemo wakili ambaye angelipwa na pesa za umma,” alifafanua Bi Achani.

Bi Achani alisema alishauriana na Spika wa Bunge la Kwale ambaye pia ni wakili kudhibiti biashara ya muguka badala ya kupiga marufuku.

Gavana huyo alisema Bunge la Kaunti ya Kwale lilichukua maoni na kupitisha mswada ambao umeongeza ada za biashara ya muguka lori tani 15 na zaidi atatakiwa Sh300,000, tani saba hadi tani 15 kiasi cha Sh200,000 na tani tano hadi saba Sh150,000.

Ada nyingine ni gunia Sh20,000, beseni Sh10,000, na tuktuk Sh40,000 na leseni ya kuuza muguka na miraa ni Sh50,000.

Hata hivyo, alisema hajatia saini mswada huo.

“Tunataka yule ambaye ametengeneza biashara yake kwenye mti akiuza muguka au miraa alipe leseni ya Sh50,000. Tukiweka hivi watu wengi hawatauza muguka na wale watauza, wataweka bei ya juu,” aliongeza.

Bi Achani alisema ada hizo zitahakikisha mtoto wa Kwale hawezi kupata muguka kwa urahisi.

Akiongea kwenye mahojiano na kituo cha redio jijini Mombasa, Bi Achani alisisitiza kuwa haungi mkono utumizi wa muguka.

Hata hivyo alijitetea akisema sheria inamfunga dhidi ya kuharamisha biashara hiyo katika kaunti ya Kwale.

“Uwezo wangu kama gavana ni kuweka mikakati ya kudhibiti utumizi wa muguka. Lakini tunapoweka mikakati ya kudhibiti pia tunawaelezea wabunge wetu kuweka sheria bungeni kupiga marufuku utumizi wa majani hayo,” alisema.

Alisema hali ya afya ya vijana wa Kwale imemshurutisha kuanza vita dhidi utumizi wa muguka.

Bi Achani alisema alipata msukumo wa kuharamisha muguka hata hivyo alisimama kidete na kukataa akionya kuwa huenda angelishtakiwa kwa mujibwa kisheria kama wenzake Bw Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi) na Andrew Mwadime (Taita Taveta).

Watatu hao walishtakiwa na wafanyibiashara kwa kupiga marufuku biashara hiyo ndani ya kaunti zao. Hata hivyo mahakama ya Embu iliondoa marufuku hayo.