Acheni siasa za chuki na ukabila, Wetang’ula aambia viongozi
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesisitiza azma ya serikali ya Kenya Kwanza ya kuboresha miundombinu kote nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuwezesha vijana na wanawake.
Spika huyo aliwahimiza viongozi wa kitaifa kuepuka siasa za chuki, matusi na ukabila, na badala yake kuhimiza umoja wa kitaifa.
“Wakenya wanapaswa kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto. Vijana wajipange katika makundi ili kufaidika kupitia mpango wa Nyota unaotoa mafunzo na msaada wa kifedha kwao,” alihimiza.
Akihutubia wakazi wa eneobunge la Teso Kaskazini, Bw Wetang’ula alisema serikali imeweka miundombinu kama mojawapo ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi, akithibitisha kuwa fedha tayari zimetengwa kwa ujenzi na upanuzi wa barabara kuu ya Malaba–Nairobi.
“Mradi huu unalenga kupunguza msongamano wa malori hadi hapa mpakani Malaba. Tunaelewa uwezo mkubwa wa kibiashara katika eneo hili la mipakani,” alisema Wetang’ula.
Alifichua kuwa ujenzi tayari umeanza katika eneo la Rironi, akisema Rais William Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wamejitolea kuwezesha biashara na usafirishaji huru wa watu, bidhaa na huduma kati ya mataifa hayo jirani.
“Mpango huu utaruhusu wananchi wa Kenya na Uganda kutangamana kwa uhuru zaidi, kufanya biashara bila vikwazo na kuishi kwa maelewano,” aliongeza Wetang’ula.
“Wanawake wamesimama katikati ya mafanikio haya. Tukiwapatia nyenzo sahihi, maarifa na fursa, tutajenga familia zenye ustawi na kukuza uchumi shirikishi kote nchini,” alisema.
Alisisitiza kuwa viongozi thabiti ni wale wanaofanya maamuzi magumu kwa lengo la kuleta mabadiliko kwa maisha ya wananchi.