Achezea majirani rafu?
NA WANDERI KAMAU
MBINU za kijanja za kutekeleza sera za kigeni na kiuchumi za serikali yake zimemfanya Rais William Ruto kutengwa na mataifa jirani, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa marafiki wa Kenya.
Chini ya utawala wake, Kenya imejipata kwenye mivutano ya kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi na karibu majirani wake wote, hali inayozua wasiwasi kuhusu mustakabali wa mahusiano baina yake na mataifa hayo.
Ingawa wadadisi wanasema kwamba Rais Ruto analenga kuona Kenya ikidumisha nafasi yake kama kiongozi wa uchumi katika ukanda huu, mbinu anazotumia zinamfanya atengwe na wenzake.
“Nia ya Rais Ruto na serikali yake ni kuendelea kudumisha ushawishi wa Kenya kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na barani Afrika kwa jumla. Hata hivyo, lazima Rais atahadhari, ili asionekane kuvuruga urafiki na ujirani ambao umekuwepo kwa muda mrefu,” akasema Prof Macharia Munene, ambaye ni mtaalamu wa siasa za kimataifa.
Anasema kuwa kiini cha Rais Ruto kuonekana kutengwa na wenzake katika ukanda huu ni juhudi zake za kuendelea kujidhihirisha kama kiongozi wa taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi na kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Baadhi ya nchi ambazo zimekwaruzana na Kenya ni Tanzania, Uganda, Sudan, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mnamo Januari 15, 2024, Tanzania ilitangaza kusimamisha safari zote za ndege kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam kuanzia Januari 22, 2024. Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Kusimamia Safari za Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa hilo lilifuatia hatua ya Kenya kukataa ndege za kubeba mizigo kutoka shirika la Air Tanzania kusafiri Kenya.
“Hili ni jibu kwa Kenya kufuatia hatua yake kukataa ombi la shughuli zote za ndege za kubebea mizigo kutoka Air Tanzania, kati ya Nairobi na Dar es Salaam,” akasema Johari.
Hata hivyo, Tanzania ilitangaza kubatilisha uamuzi huo baadaye “baada ya makubaliano baina yake na Kenya”.
Mwanzoni mwa Januari, Uganda iliishtaki Kenya katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu Haki (EACJ), ikidai kuwa Kenya imekataa kuipa leseni ya kusafirisha mafuta yake kutoka bandari ya Mombasa hadi Uganda.
Uganda ilidai kwamba Kenya inakiuka makubaliano ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu baina ya mataifa hayo kuhusu usafirishaji wa bidhaa hiyo.
Mnamo Januari 4, 2024, Sudan ilimwagiza balozi wake Kenya kurejea nchini humo, baada ya Rais Ruto kufanya mazungumzo na kiongozi wa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF), Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, linalokabiliana na jeshi la taifa hilo kuhusu udhibiti wa maeneo muhimu, kama vile jiji la Khartoum.
Kwenye taarifa, serikali ya Sudan ilitaja mazungumzo hayo kama yanayoonesha “mwegemeo wa Kenya kuhusu mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea nchiwni humo”. Mzozo huo haujasuluhishwa hadi sasa.
Mnamo Desemba 15, 2023, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilimwagiza balozi wake nchini Kenya kurejea katika nchi hiyo, baada ya viongozi kadhaa wa upinzani kuzindua muungano mpya wa makundi ya waasi jijini Nairobi.
Uzinduzi wa kundi hilo -Congo River Alliance (CAR) -ulifanywa siku kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa taifa hilo uliofanyika Desemba 20, 2023.
DRC ilisema ilichukua hatua hiyo ikizingatiwa kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo yamepeleka kikosi cha majeshi kudumisha amani nchini humo.
Mnamo Desemba, Kenya pia ilitofautiana vikali na Somalia, baada ya Spika wa Seneti Amason Kingi kudai kwamba Kenya ina “urafiki mkubwa na eneo la Somaliland”.
Baadaye, Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei alitaja kauli ya Bw Kingi kama ambayo “haikuashiria msimamo wa Kenya katika kuitambua Somaliland kama taifa huru”.
Kutokana na tofauti hizo, wadadisi wa siasa na mahusiano ya kimataifa wanasema kuwa lazima Kenya ianze kutahadhari kuhusu mustakabali wa uhusiano wake na mataifa hayo.
Prof Munene alisema kuwa kuna wakati ambapo Kenya itahitaji uungwaji wa mataifa hayo kuwania nafasi yoyote kimataifa, kwa mfano katika Umoja wa Mataifa (UN), hivyo si taswira nzuri inapoonekana kuingilia migogoro ya kisiasa au masuala ya ndani katika mataifa hayo.
Kwa upande wake, Prof Peter Kagwanja, anaonya kwamba huenda tofauti hizo zikazua migawanyiko katika EAC, hali ambayo inaweza ikavuruga mustakabali wa jumuiya hiyo.
“Tunafaa kufahamu kuwa jumuiya hiyo ilianguka nyakati za marehemu Julius Nyerere na Daniel arap Moi. Jumuiya iliyopo ni baada ya kufufuliwa upya. Tunafaa tutahadhari sana kurejea hapo, hasa mataifa mengi zaidi yanapoendelea kujiinga nayo,” akasema Prof Kagwanja.