Habari za Kitaifa

Afisa aliyeuawa Ikulu Matanka na mshukiwa Kimunyi walikuwa marafiki, uchunguzi wabaini

Na KAMORE MAINA, RICHARD MUNGUTI, STANLEY NGOTHO October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAMADHAN Matanka, 30, aliyeuawa akilinda Ikulu ya Nairobi Jumatatu, alikuwa tayari amewahudumia Marais wawili tofauti wa Kenya katika nyadhifa tofauti, kwa kipindi cha miaka mitatu.

Matanka alipata kazi yake ya kwanza Ikulu mnamo mwaka wa 2020. Baba yake, Hassan Dabie Matanka, alikuwa mfanyakazi wa Ikulu.

Rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta, alitoa agizo kuwa watoto wa wafanyakazi wa Ikulu waliokuwa wametimu umri wa miaka 18 waajiriwe katika mradi wa kusafisha Mto Nairobi na kusaidia katika usimamizi wa taka jijini.

Kazi ya kwanza ya wafanyakazi waliofahamika kama Green Army ilikuwa kusafisha Ikulu vizuri – na ilikuwa pia njia ya kuwakinga vijana hao dhidi ya athari mbaya za mitaani. Wakati huo, Matanka alikuwa amemaliza mtihani wake wa KCSE.

Vyanzo kadhaa vya karibu na uchunguzi wa mauaji ya kikatili ya Matanka vilifichua kuwa alikutana na Kithuka Kimunyi – mshukiwa wa mauaji – alipokuwa kwenye Green Army.

Kwa sasa, Kimunyi anazuiliwa kwa siku 14 kuhojiwa na polisi. Matanka alizikwa Jumanne nyumbani kwao Kajiado kwa mujibu wa desturi za Kiislamu.

Inaaminika kuwa Matanka na Kimunyi walianza urafiki wa karibu, licha ya tofauti ya umri – Kimunyi akiwa na miaka 56, mara mbili ya umri wa Matanka.

Katika mojawapo ya mazungumzo kati ya Rais na wanachama wa Green Army, aliwauliza kama kuna yeyote aliyekuwa na hamu ya kujiunga na Huduma ya Kitaifa ya Polisi. Matanka alikuwa mmoja wa wale waliotangaza nia kwa kuinua mkono wake kwa ujasiri.

Ndipo alipopata nafasi ya kujiunga moja kwa moja na Kikosi cha GSU.

Hatimaye, aliteuliwa kujiunga na kikosi maalum kinachotoa ulinzi Ikulu na makazi ya Rais kote nchini.

Mnamo Julai 2025, Matanka alihamishiwa Ikulu ya Nairobi kama afisa wa ulinzi chini ya utawala wa Rais wa sasa, Dkt William Ruto. Kazi yake ilikuwa kuchunguza wageni na magari yanayoingia kupitia malango mbalimbali ya Ikulu.

Alikuwa mstari wa kwanza wa ulinzi endapo kungetokea tishio lolote la usalama.

Wakati Matanka alirejea Ikulu kama afisa wa GSU, mkataba wa Kimunyi ulikuwa umeisha. Lakini urafiki wao uliendelea.

Mara kwa mara, Matanka na Kimunyi walikutana katika milango tofauti ya Ikulu kulingana na ni lango lipi Matanka alikuwa akilinda siku hiyo. Polisi sasa wanadai kuwa Jumatatu, Kimunyi alificha mshale kwenye gunia na aliingia katika kibanda cha ulinzi cha Lango D la Ikulu, na kumpiga Matanka kwa mshale kifuani hadi kumuua.

Maafisa wawili wenzake Matanka waliokuwa wakikagua gari wakati tukio lilipotokea, wametoa taarifa kwa DCI. Wameeleza kuwa urafiki kati ya Matanka na Kimunyi ulikuwa wa wazi, na hata waliruhusiwa kuketi pamoja ndani ya kibanda cha ulinzi jambo ambalo kawaida ni kosa la kiusalama.

Afisa mmoja anayehusishwa na uchunguzi alieleza kuwa picha za CCTV, ambazo sasa zinachunguzwa na DCI wa Kilimani, zilionyesha mazungumzo kati ya Matanka na Kimunyi yalidumu kwa takriban dakika 17 kabla ya tukio.

“Baada ya kuangalia CCTV, tunasema wazi kulikuwa na uzembe mkubwa kwa upande wa maafisa,” alisema mpelelezi huyo.

Katika video hiyo, inaonyeshwa kuwa maafisa wenzake waliondoka wakimuacha Matanka akiendelea kuzungumza na Kimunyi.

Ndipo mshukiwa alichomoa mshale na kumdunga Matanka, ambaye alianguka chini.

Uchunguzi huu ni tofauti na taarifa ya awali ya Huduma ya Polisi, ambayo ilisema kwamba mtu mwenye silaha aliyekuwa akizurura alifyatua mshale baada ya kuonywa na maafisa wa usalama.

Kimunyi sasa anazuiliwa kwa siku 14 kwa agizo la mahakama ya Nairobi, wakati uchunguzi unaendelea.

Afisa mmoja wa DCI aliliambia gazeti la Taifa Leo kuwa Kimunyi bado hajatoa maelezo kamili ya mauaji hayo, na badala yake anadai kuwa alichochewa na “nguvu za giza”.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja alisema hawezi kutoa taarifa kwa sasa hadi uchunguzi utakapokamilika:

“Tusubiri uchunguzi ukamilike ndipo tuelewe kilichotokea,” alisema kwa njia ya simu.

Wakati huohuo, Kamanda wa GSU Robinson Lolomodon amewaagiza maafisa wa juu wa polisi wanaolinda Ikulu kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.