• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Afisa wa polisi anayetaka apewe kazi ya kuhubiria wenzake na vijana

Afisa wa polisi anayetaka apewe kazi ya kuhubiria wenzake na vijana

NA RICHARD MUNGUTI

AFISA wa Polisi ameisihi Mahakama ya Nairobi imruhusu aanze kuhubiria vijana na maafisa katika idara ya polisi kujiepusha na uhalifu badala ya kumhukumu kifo baada ya kupatwa na hatia katika wizi wa mabavu ambapo alimnyang’anya Keshia Daksh Patel Dola 150,000 (KSh15 milioni) Desemba 2020.

Koplo George Onyango Mtere alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bernard Ochoi “nimejitolea mhanga kuhubiria vijana na maafisa wenzangu katika idara ya polisi wajiepushe na uhalifu.”

Koplo Mtere alisema atakuwa mtu wa maana akifungwa nje badala ya kuhukumiwa kunyongwa jinsi korti ilivyoombwa na kiongozi wa mashtaka James Gachoka.

Akichambua ripoti za afisa wa urekebishaji tabia, stetimenti ya chifu, afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Ruiru, walalamishi na ripoti ya idara ya sheria na haki (NCAJ) Wakili Danstan Omari alimweleza hakimu “Koplo Omnyangu atakuwa wa manufaa akiwa nje kuliko akiwa gerezani.”

Akiililia mahakama impe kifungo cha nje, Bw Omari alisema Koplo Onyango mwenye umri wa miaka 49 na baba wa watoto watano ameghairi matendo yake na yuko tayari kutumikia jamii katika kiwango kingine.

Wakili huyo alisema kwamba mshtakiwa ametumikia nchi hii akiwa afisa wa polisi kwa miaka 25.

“Koplo Onyango amehudumia nchi hii akiwa afisa wa polisi. Amepambana na magaidi wa Al Shabaab. Amechapana na wahalifu. Hajawahi fikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya Idara ya Polisi. Idara ya Urekebishaji tabia imewahoji watu kadhaa, wakiwemo Chifu wa Lokesheni ya kwao na aliyekuwa mkubwa wake kituo cha polisi cha Ruiru na wote wameomba mahakama impe kifungo cha nje kwa vile ni mtu mwema,” Bw Omari alisimulia.

Pia alisema mlalamishi Dakshi Patel alimsamehe na kueleza mahakama hakutumia vibaya bastola aliyokuwa nayo.

Kile ambacho Dakshi aliomba ni pesa zilizopatikana arudishiwe.

Bw Omari alieleza mahakama kwamba Pasta wa kanisa analohudhuria Koplo Onyango alikiri mshtakiwa huwashauri vijana kanisani jinsi ya kuwa waadilifu.

Wakili huyo alieleza mahakama kwamba mshtakiwa anaugua maradhi yanayotishia maisha na akisukumwa jela “ni sawa na kuzikwa kaburini kwa vile idara ya magereza imeungama kwamba haina dawa za kutibu magonjwa kama vile Kansa, Kisukari na shinikizo la damu.”

Akiomba korti iige mfano wa Mahakama Kuu ya Mombasa ambapo Jaji alimwamuru Padri arudi kanisani kuwaelezea waumini athari za kushiriki ngono, Bw Omari alisema Koplo Onyango ni heri akiwa nje badala ya kusukumwa gerezani.

Wakili mwingine Gordon Ogado aliungana na Bw Omari kueleza mahakama kwamba wateja wake wanne walioshtakiwa pamoja na Koplo Onyango wanahitaji kufungwa nje tu.

Lakini kiongozi wa mashtaka James Gachoka aliomba mahakama iwahukumu Koplo Onyango na Bernard Ogutu Okech kifo kwa wizi wa mabavu wakitumia bastola.

“Tayari hii mahakama imewapata na hatia na adhabu iliyopo ni moja tu – kifo kwa vile washtakiwa walitumia silaha hatari kumtisha keshia awache mfuko uliokuwa na pesa,” alisema Bw Gachoka.

Bw Gachoka alisema afisa huyo alitumia bastola kumtishia Dakshi Patel – mfanyakazi wa kampuni ya Mitsumi Computer Garage.

Alipoona bastola Dakshi alishtuka na kutupa chini mfuko uliokuwa na pesa.

Hakimu aliwazuilia washtakiwa hao hadi Aprili 17, 2024 atakapopitisha hukumu.

 

  • Tags

You can share this post!

Afueni KPLC ikishusha bei ya umeme kwa hadi asilimia 13.7

Bwanyenye adinda kufika kortini kujibu kesi ya wizi wa...

T L