Afisa wa polisi au mwenzake kwa kumsukuma kutoka orofa wakizozania mpenzi
Maafisa wa upelelezi katika mji wa Kitengela, Kaunti ya Kajiado, wanamzuilia afisa wa polisi anayedaiwa kumsukuma mwenzake hadi kufa kutoka orofa ya nne ya jumba moja usiku wa Alhamisi, wakizozania mpenzi.
Kulingana na ripoti ya polisi, konstebo wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kitengela alikuwa amemtembelea mpenzi wake mwenye umri wa miaka 27 katika mnamo saa kumi na mbili jioni. Alikuwa amesafirishwa kwa pikipiki na mhudumu aliyewaambia polisi kwamba alikuwa amepangiwa kumchukua baadaye usiku.
Wakiwa ndani ya nyumba, mpenzi mwingine wa mwanamke huyo, sajini wa polisi kutoka Kitengo cha Ulinzi wa Miundomsingi Muhimu (CIPU) katika eneo la EPZ, alifika nyumbani hapo na hali ikabadilika ghafla kuwa vita.
“Wakiwa ndani, mwanaume mwingine ambaye alibainika kuwa afisa wa polisi kutoka kambi ya CIPU EPZ Athi River – pia mpenzi wa mwanamke huyo – alifika nyumbani kwake, ambapo inadaiwa mzozo ulizuka kati ya maafisa hao wawili, na marehemu akazidiwa nguvu na kusukumwa kutoka nyumba kupitia roshani hadi chini na kufariki papo hapo,” ilisema sehemu ya ripoti ya polisi.
Jirani mmoja aliyefichua habari hizo kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema mwanzoni wapenzi hao walikataa kufungua mlango lakini kuugonga kwa hasira kulikofanywa na mwanaume wa pili kulivutia majirani waliokuwa wakitazama.
“Tulikuwa tukisikia kelele kutoka ndani ya nyumba. Marehemu alizidiwa nguvu na kusukumwa hadi kwenye roshani kabla ya kuanguka hadi chini,” alisema jirani huyo, ambaye pia alisema wanaume hao wawili walikuwa wageni wa mara kwa mara wa mwanamke huyo, akisema ni kuwa mtu anayehusiana kimapenzi na zaidi ya mwanamume mmoja kwa wakati mmoja.
Afisa huyo wa polisi alifariki papo hapo, na mwili wake ulipelekwa hadi Hospitali ya Shalom na maafisa wenzake mwendo wa saa nne usiku baada ya uchunguzi wa eneo la tukio kukamilika.
Washukiwa wawili afisa wa polisi na mwanamke huyo wanazuiliwa na polisi huku wakisaidia katika uchunguzi unaoendelea.
Kamanda wa Polisi wa Isinya, Simon Lomitari, alisema maafisa hao wote wawili walikuwa wamevaa mavazi ya kiraia na hawakuwa na silaha wakati tukio lilipotokea.
“Ni tukio la kusikitisha lakini tunalichunguza kwa haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Lomitari.