Habari za Kitaifa

Afisi ya Gachagua yamulikwa kwa mapazia ya Sh10m

February 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PETER MBURU Na CHARLES WASONGA

KWA upande mmoja serikali ikiendelea kulaumiwa kwa kuwabebesha Wakenya mzigo mzito wa ushuru, upande huo mwingine inamulikwa kwa kuendeleza ubadhirifu wa fedha hizo kupitia ununuzi wa bidhaa zisizo na faida kwa Wakenya.

Ripoti ya hivi punde ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, imefichua kuwa afisi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua ilinunua mapazia ya thamani ya Sh10.27 milioni mwaka 2023 pekee.

Kwa ujumla, afisi hiyo ilitumia kitita cha Sh18.14 milioni kwa ununuzi wa mapazia na fanicha katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2023.

Hii ina maana kuwa fedha zilizotumika kununua mapazia pekee (Sh10.27 milioni) zinaweza kutumika kununua nyumba 12 chini ya mpango wa serikali wa nyumba za gharama nafuu ikizingatiwa kuwa nyumba ya bei ya chini zaidi itauzwa kwa Sh840,000.

Nyumba kama hizi ni zile ambazo ziko katika kitengo cha nyumba za kijamii (Social Housing) zinazolenga kufaidi Wakenya wenye mapato ya chini ya Sh20,000 kila mwezi.

Pesa zilizotumika kununua mapazia (Sh10.27 milioni) katika makazi ya Bw Gachagua pia zinaweza kutosha nyumba 10 za chumba kimoja cha kulala chini ya Mpango huo wa Nyumba za Gharama Nafuu katika kategoria ya Wakenya wenye mapato ya kati ya Sh20,000 na Sh150,000 kila mwezi.

Ufichuzi huo wa Bi Gathungu unajiri baada ya ripoti ya Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o kufichua kuwa serikali kuu ilitumika Sh600 milioni kugharimia ukarabati wa Makazi Rasmi ya Naibu Rais katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Shughuli hiyo iliendeshwa kuanzia Septemba 13, 2022, baada ya kuapishwa kwa Bw Gachagua na Rais William Ruto kufuatia ushindi wao katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Ubadhirifu unafichuliwa serikalini wakati ambapo Wakenya wanaendelea kuzongwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Kwa upande wake, serikali kuu inadai uchumi unaimarika kufuatia kupungua kwa bei za vyakula na kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani.

“Katika mwaka ambapo ukaguzi ulifanywa, Afisi ya Naibu Rais ilinunua mapazia na fanicha za thamani ya Sh10,272,524 na Sh7,869,700, mtawalia. Ununuzi huo wote uligharimu Sh18,142,224 zilizoagizwa wakati wa ununuzi huo tofauti,” Bi Gathungu akafichua kwenye ripoti yake.

“Hii ilikuwa ni kinyume cha Sehemu ya 54 (1) ya Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma wa 2015 inayosema kuwa hakuna asasi itakayoruhusiwa kugawanya ununuzi kuwili kwa lengo la kukwepa taratibu zilizowekwa,” akaongeza.

Ripoti ya Bi Gathungu pia inafichua kuwa Afisi ya Naibu Rais alikosa kulipa Sh58.2 milioni kwa wafanyabiashara walioiuzia bidhaa na huduma katika kipindi hicho cha hadi Juni 30, 2023.

Kwa hivyo, deni hilo lilipitishwa hadi kwa mwaka wa kifedha wa sasa wa 2023/2024.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pia ilifichua visa ambapo baadhi ya wafanyabiashara waliowasilisha bidhaa kwa afisi ya Bw Gachagua walilipwa hata kabla ya afisi hiyo kuagiza huduma.

Afisi hiyo ilinunua bidhaa na huduma za thamani ya Sh198.6 milioni katika kipindi hicho, huku afisi ya Bi Gathungu ikibaini dosari katika stakabadhi zilizotumika katika ununuzi huo.

“Stakabadhi zilizowasilishwa kwa ukaguzi zilionyesha tarehe tofauti kuanzia wakati wa kuanzishwa, kutayarishwa na kulipiwa kwa bidhaa hizo. Hii ni kinyume cha Sehemu ya 53 (1) ya Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali ya Umma, 2015 inayosema kuwa shughuli zote za ununuzi za asasi za serikali ni sharti kuzingatia kanuni na taratibu za Sheria hiyo,” Bi Gathungu akaeleza katika ripoti yake.

Afisi ya Naibu Rais pia ilikoselewa kwa kununua fanicha za thamani ya Sh2.4 milioni moja kwa moja bila kutangaza zabuni jinsi inavyohitaji kisheria.

Ununuzi wa moja kwa moja huruhusiwa kwa bidhaa na huduma za usalama zinazonunuliwa kutoka kwa wafanyabiashara wachache pekee.