• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Afueni KPLC ikishusha bei ya umeme kwa hadi asilimia 13.7

Afueni KPLC ikishusha bei ya umeme kwa hadi asilimia 13.7

NA CHARLES WASONGA

DALILI kwamba gharama ya maisha itaendelea kupungua katika siku za hivi karibuni imeonekana saa chache baada ya bei ya mafuta kushuka kwa kiwango kikubwa.

Jumatatu, Aprili 15, 2024 Kampuni ya Usambazaji Umeme Nchini (KPLC) ilitangaza kuwa imeteremsha bei ya kawi hiyo kwa kima cha asilimia 13.7.

“Hii ina maana kuwa mteja chini Kategori ya Nyumba anayetumia nguvu ya umeme isiyozidi vipimo 30 kila mwezi atalipa Sh629 mnamo Aprili 2024 ikilinganishwa na Sh726 alizolipa Machi 2024 kwa vipimo sawa na hivyo.

Kwenye taarifa kampuni hiyo ilisema hatua hiyo inachangiwa na kupunguzwa kwa bei ya mafuta na kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Kenya.

“Ada kuhusu gharama ya mafuta na mabadiliko ya thamani ya sarafu za kigeni ambazo ni sehemu kuu katika bili ya stima, imepungua kwa asilimia 37.3 kati ya Machi 2024 na Aprili 2024 kulingana na mwongozo wa bei uliotolewa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (Epra),” KPLC ikasemna.

Kulingana na kampuni hiyo, ada ya gharama ya mafuta imepungua kutoka Sh4.64 kwa lita mnamo Machi 2024 hadi Sh3.26 Aprili 2024. Ada hiyo ilikuwa Sh4.93 mnamo Januari mwaka huu, 2024.

Vile vile, ada ya mabadiliko ya thamani ya sarafu za kigeni imepungua kutoka Sh3.68 mnamo Machi 2024 hadi Sh1.96 Aprili 2024.

Ada hiyo ilikuwa imefikia kiwango cha Sh6.85 kwa kila lita ya mafuta Januari 2024.

“Kupungua kwa ada hizo kumeleta afueni kwa wateja wetu. Isitoshe, kufuatia mvua kubwa inayonyesha kote nchini wakati huu KPLC itazalisha kawi nyingi kwa njia ya maji na kutotegemea zaidi kawi inayozalishwa kwa mitambo inayotumia mafuta,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa KPLC Joseph Siror.

Kulingana na punguzo hilo wateja wanaotumia vipimo 60 kila mwezi atalipa Sh1,574 mwezi Aprili 2024 ikilinganishwa na Sh1,773 Machi 2024.

Hii inawakilisha punguzo la bei ya stima kwa kima cha asilimia 11.2.

Nao wateja wanaotumia vipimo 120 vya stima kila mwezi, watalipa Sh3,728 mwezi huu (Aprili) ikilinganishwa na Sh4,127 walizolipa mwezi jana, hii ikiwakilisha punguzo la kima cha asilimia 9.7.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Peter Kenneth ‘aoga’ na kurejea sokoni

Afisa wa polisi anayetaka apewe kazi ya kuhubiria wenzake...

T L