Habari za Kitaifa

Afueni kwa Super Metro marufuku ya NTSA ipigwa breki

Na SAM KIPLAGAT March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BODI ya Rufaa ya Uchukuzi na Leseni Jumatano, Machi 24, 2025 iliondoa marufuku ya muda iliyokuwa imewekea kampuni ya mabasi ya Super Metro inayoendesha shughuli zake Nairobi na viungani mwa jiji hilo.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt Adrian Kamotho, aliondoa marufuku hiyo iliyowekwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi Barabarani (NTSA) wiki jana.

Aidha, aliamrisha kampuni hiyo irejelee shughuli zake kwa kuzingatia sheria.

“Kwamba amri hii inastahili kuwasilishwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi,” ikasema amri ya jopo hilo likiondoa marufuku hiyo.

NTSA iliondoa leseni ya Super Metro kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inatii na kuzingatia masharti yote ya usalama kulinda abiria wake na watumiaji wengine wa barabarani.

Hata hivyo, Super Metro ilipinga marufuku hiyo ikisema haikupewa notisi ya mashtaka dhidi ya tukio lolote kuanzia Januari hadi Machi 2025.

Pia, NTSA haikuipa Super Metro nafasi ya kusikilizwa au kujitetea kabla ya kutoa uamuzi huo au kuondoa leseni yake kwa muda.

“Hakuna sababu yoyote yenye mashiko kuondoa leseni kwa sababu wamezingatia matakwa yote ya kisheria. Juhudi zozote za kuondoa leseni hizo zinatokana na sababu za nje,” ikajitetea Super Metro.

Super Metro ilisema kuwa barua ya Machi 18, NTSA ilizungumzia ajali za barabarani zilizoishia kwa mauti ambazo hazikufahamishwa ilhali matukio hayo ndiyo yalikuwa msingi wa kupokonywa kwao leseni.

Walidai kuondolewa kwa leseni hakukufaa na ilikuwa inalenga kutoa taswira mbaya kwa utendakazi wa Super Metro na kuwasababishia hasara.

“Ajali zinazorejelewa hazikusababishwa na kampuni bali watu binafsi na kuchangia Super Metro kukashifiwa,” ikaongeza kampuni hiyo.

Dkt Kamotho aliamrisha suala hilo lisikilizwe mnamo Machi 27 mwaka huu.

Kampuni hiyo ya uchukuzi, imekuwa ikishambuliwa mitandaoni kwa utepetevu barabarani hasa baada ya makanga wa mojawapo ya mabasi yake kudaiwa kurusha nje abiria gari likiwa kwa mwendo wa kasi.

Abiria huyo alifariki papo hapo.

Hata hivyo, kampuni hiyo na wafanyakazi wake wamekanusha kuhusika kwa kisa hicho cha unyama.