Afueni kwa wake wa pili wakipata idhini kuzika mume
NA RICHARD MUNGUTI
MKE wa pili katika ndoa yenye zaidi ya bibi mmoja sasa atakuwa huru kuzika mumewe.
Afueni hii kwa wake wa pili, imetokana na uamuzi wa kihistoria ambapo kesi iliyohusisha mume aliyeaga akiwa na umri wa miaka 100 mkewe wa pili ameruhusiwa na korti kumzika.
Mahakama ya Milimani imezindua ukurasa mpya katika kesi za kupigania mtu akiwa ameaga, ikiamuru mmoja awe akizikwa na mke ambaye amekuwa akiishi naye kabla ya kuaga.
“Mtu akifa ana haki ya kuzikwa na mke waliyekuwa wakiishi naye kabla ya kuaga,” hakimu mwandamizi Bw Gerald Gitonga alisema huku akimruhusu Sarah Kathambi, 78, kumzika Silas Kamuta Igweta, 100.
Kamuta ambaye mwili wake umehifadhiwa katika Mochari ya Ummash aliaga Feburuari 17, 2024.
Kabla ya kufariki, alikuwa akiishi na Sarah katika makazi yao ya kifahari Westlands, jijini Nairobi.
Mke wa kwanza, Grace Rigiri waliyekuwa wamefunga ndoa naye kanisani, aliwasilisha kesi kortini akipinga Sarah kumzika.
Grace alisema ndiye alikuwa na haki ya kumzika mumewe kama mke wa kwanza.
Mjane huyo alikuwa anaomba aruhusiwe kumzika Kamuta katika shamba lake Embu.
Lakini Sarah kupitia mawakili Nelson Kinyanjui, Danstan Omari na Shadrack Wambui alipinga hatua ya Grace akisema, Kamuta alikuwa amemweleza akiaga amzike yeye (Sarah) na watoto wake.
Mahakama ilielezwa na Bw Omari kwamba sheria za Kenya hazijafafanua sehemu ambayo mwanamume mwenye zaidi ya mke mmoja anapaswa kuzikwa.
Mawakili hao walimsihi Bw Gitonga amruhusu Sarah amzike mumewe waliyeishi pamoja kwa zaidi ya miaka 40.
“Kwa miaka zaidi ya 40 Kamuta hakuishi na Grace. Ukweli ni kwamba Grace hamfahamu mumewe waliyefunga ndoa kanisani, lakini wakatalikiana ndipo Sarah akaolewa kwa mujibu wa sheria za Utamaduni wa Ameru,” Bw Omari alisema, akimsihi hakimu abadilishe mkondo wa sheria za mazishi.
Wakili Omari alisema maiti ina haki ya kuzikwa pale mwendazake alichagua akiwa hai.
Akitoa uamuzi, Bw Gitonga alisema chini ya sheria za haki za wafu mmoja anatakiwa kuzikwa na wale aliokuwa akiishi nao.
Lakini familia ya Grace iliwasilisha ombi la kusitisha mazishi kwa siku 14 kukata rufaa katika mahakama kuu.
Hata hivyo, mawakili Kinyanjui, Omari na Wambui wametoa wito kwa familia ya Grace iruhusu mazishi yafanywe kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama.
Aidha, uamuzi huu umezindua sura mpya kuhusu zoezi la mazishi na haki za watu wenye zaidi ya mke mmoja ambapo wanapaswa kuzikwa.