Afueni kwa Wakenya bei ya mafuta ikishuka
NA WANDERI KAMAU
MAMLAKA ya Kudhibiti Bei ya Kawi na Petroli (Epra) imetangaza kupunguzwa kwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa mtawalia.
Kulingana na taarifa ambayo Epra imetoa Alhamisi, bei ya petroli ilishuka kwa Sh7.21, dizeli Sh5.09 huku mafuta taa yakishuka kwa Sh4.49.
Kutokana na hatua hiyo, inamaanisha kuwa jijini Nairobi, lita moja ya petroli itakuwa ikiuzwa kwa Sh199.15, dizeli Sh190.38 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh188.74.
Mamlaka ilisema kuwa bei hizo mpya zitatekelezwa kuanzia leo, Alhamisi, Machi 15, 2024, usiku wa manane, hadi Aprili 14, 2024.
“Bei hizo zinajumuisha asilimia 16 kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kulingana na Sheria ya Fedha 2023 na Sheria za Ushuru (Marekebisho) 2020,” ikasema mamlaka hiyo kwenye taarifa.
Jijini Mombasa, lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh195.97, dizeli Sh187.21, huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh185.58 mtawalia.
Hapo awali, Rais William Ruto alikuwa amewaahidi Wakenya kwamba bei za mafuta zingeshuka.
Bei za mafuta nchini zinashuka wakati bei hizo zinapanda katika sehemu nyingine duniani, baada ya mataifa yanayozalisha mafuta kukubali kuendelea kupunguza uzalishaji wake kila siku kwa mapipa 2.2 milioni hadi Juni.
Wakenya kadhaa waliozungumza na Taila Leo walitaja hali hiyo kama ishara kwamba huenda hali ngumu ya kiuchumi iliyopo nchini ikaanza kuimarika.
Bw Jack Kasyoka, ambaye ni mkazi wa Juja, Kaunti ya Kiambu amesema huo ni mwelekeo mzuri.
“Ni hali inayoashiria kuwa hatimaye, huenda mambo yakaanza kuimarika nchini, kinyume na jinsi wengi walivyotarajia,” akasema Bw Kasyoka.
Ijapokuwa hakuna sababu zozote zilizotolewa kuhusiana na mwelekeo mpya kuhusu kushuka kwa bei hizo, baadhi ya wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanauhusisha na kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni katika siku za hivi karibuni.