Aibu wabunge wanawake wakilimana
WABUNGE wawili wa kike, Umulkher Harun Mohamed, Mbunge mteule wa chama cha ODM, na Falhada Iman, mwakilishi wa UDA katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), waligombana na kupigana wakiwa Bungeni jijini Nairobi.
Tukio hilo lilitokea Jumanne mchana, Aprili 8, 2025 mbele ya macho ya viongozi wengine na walinzi wa Bunge.
Kulingana na video iliyosambazwa mitandaoni, wabunge hao walionekana wakirushiana mangumi na kuangushana chini, kabla ya baadhi ya viongozi kuingilia kati kuwatenganisha.
Baada ya tukio hilo kuzua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na kulaaniwa vikali na wananchi pamoja na mashirika ya kijamii, mbunge Umulkher alitoa taarifa kupitia mitandao yake ya kijamii akiomba umma msamaha.
“Leo, tukio la kusikitisha lilitokea katika viwanja vya Bunge – hali ambayo najutia sana kama mbunge na pia kama mama. Mwenzangu kutoka EALA, ambaye kwa muda mrefu amekuwa na msimamo mkali dhidi ya kazi yangu, alikuja Bungeni akiwa na nia ya kunishambulia. Tukio hili lilinitokea ghafla na kuniacha na maswali mengi kuhusu sababu ya shambulio hilo.
“Ninajutia sana tukio hili na nataka kusisitiza kuwa sishabikii wala kuunga mkono aina yoyote ya tabia isiyofaa. Ingawa sitatoa maelezo zaidi kwa sasa, ninabaki na dhamira ya kudumisha heshima na hadhi inayotarajiwa kutoka kwa taasisi yetu na mimi binafsi, hasa kama mwanamke Muislamu.”
Bi Falhada Iman, hakuwa ametoa taarifa yoyote rasmi kuhusu kisa hicho kufikia wakati wa kuchapisha taarifa.
Wananchi, wanaharakati wa kijamii, na viongozi wa kisiasa kutoka mirengo mbalimbali walilaani vikali tukio hilo, wakilitaja kama fedheha kwa heshima ya Bunge na mfano mbaya kwa taifa.
Wito umetolewa kwa Spika wa Bunge kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wote waliohusika, huku wengi wakihimiza mafunzo ya maadili kwa wabunge wote.