Aibu ya stima kumzimia Rais maikrofoni akihutubia mawaziri katika warsha
NA MARY WANGARI
ATHARI za stima kupotea mara kwa mara zilijitokeza Rais William Ruto alipolazimika kukatiza hotuba yake kwa mawaziri wakati wa warsha iliyoandaliwa Naivasha.
Mawaziri waligubikwa na sintofahamu wasijue la kufanya stima zilipopotea mara ya kwanza Kiongozi wa Taifa akiwa jukwaani akiwahutubia.
Kwenye video iliyorekodiwa na NTV Kenya, Rais anaonekana akisema, “sababu iliyofanya niwateue ni kwa sababu nilijua mna uwezo wa kufanya kazi mnayofanya,” kabla ya stima kupotea ghafla na kumgubika gizani.
Kimya kilifuata kwa muda huku Dkt Ruto akionekana akijaribu kipaaza sauti.
“Tuko hapo,” aliuza Rais kabla ya mitambo kurejeshwa na akaendelea na hotuba yake gizani.
“Kwa sababu mna kibali na kuungwa mkono name, na wale ambao wamejishughulisha hata kunitumia ujumbe wa Whatsapp kuniuliza ‘nifanyeje?’ Mnaweza kuthibitisha kuwa nimejibu,”
“Hakuna yeyote hapa atakayesema nilifanya uamuzi usiofaa kwa sababu sikuwa na mwongozo, itisha mwongozo kutoka kwa katibu wako wa wizara, waziri wako, na ikiwa bado hujaelewa, nitumie ujumbe, niandikie barua, nitakusaidia kwa sababu ufanisi wako ni wangu.”
Rais alipokuwa akielekea kukamilisha hotuba yake, stima zilipotea kwa mara ya pili na kumlazimu kuelezeza kauli yake ya mwisho akiwa amefunikwa na giza.
Tukio hilo limejiri wakati ambapo Wakenya hususan wafanyabiashara na watoaji huduma wanaotegemea stima wakikadiria hasara kuu kutokana na hali ya stima kupotea kila mara nchini.
Licha ya kutaabika kabla ya kuunganishiwa umeme na kugharamika pakubwa kutokana na bili kubwa kupindukia za umeme, Wakenya wamekuwa wakitumia muda mwingi gizani katika muda wa miezi michache iliyopita.
Udadisi uliofanywa na Taifa Leo ulifichua kuwa wateja wanaohitajika kuunganishiwa stima huorodheshwa malipo ya hadi mamilioni.
Kulingana na Muungano wa Wenye Viwanda, gharama ya umeme imeongezeka kwa asilimia 59 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita
Wateja wanahitajika kutoa kitambulisho cha kitaifa, nakala ya cheti cha KRA na ramani inayoonyesha lilipo jengo linalohitaji kuunganishwa na stima, kwa mujibu wa Kampuni ya Umeme.
Isitoshe, wanahitajika kutoa nakala ya hatimiliki ya ardhi, stakabadhi za kutafuta ardhi ili kubainisha mmiliki wa mali husika ikiwemo fomu na vyeti vya kandarasi ya kuunganishiwa stima.