Ajali: Wanafunzi wanane wa KU wahamishiwa Nairobi kwa matibabu
NA LUCY MKANYIKA
WANAFUNZI wanane wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) waliojeruhiwa vibaya katika ajali ya Jumatatu eneo la Maungu katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, wamehamishwa kutoka Voi hadi jijini Nairobi kwa matibabu zaidi.
Basi lao liligongwa ubavuni na lori la trela lililokuwa likikwepa kugongana ana kwa ana.
Majeruhi hao ambao mwanzo walipelekwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi katika Kaunti ya Taita Taveta, mapema Jumanne wamepelekwa jijini Nairobi.
Kufuatia ajali hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi 11, Naibu Chansela wa KU Paul Wainaina alifika eneo la ajali mnamo Jumatatu ambapo alifululiza hadi hospitalini kuwafariji manusura.
Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya na 34 wangali wanatibiwa katika hospitali ya Moi mjini Voi.
Basi lilikuwa na wanafunzi 54 waliokuwa wanaenda kwa ziara ya elimu mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi. Mbali na wanafunzi, wengine walikuwa ni mtaalamu wa maabara, mwenyekiti wa wanafunzi, na madereva wawili.
Kwenye taarifa ya KU, baadhi ya wanafunzi hao watahamishwa kwa matibabu zaidi jijini Nairobi.
“Kwa sasa hatuwezi kutoa takwimu kamili au majina ya wahanga lakini tunakiri yalitokea maafa. Chuo kitatoa ripoti ya kina zaidi baadaye leo (Jumanne),” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Prof Wainaina.
Aidha KU, imekita hema la kutoa taarifa muhimu na usaidizi mwingine unaohitajika, kufuatia ajali hiyo.
Manusura wa ajali hiyo, Bw Felix Onyango alisema dereva wa basi la KU alikuwa akiyapita magari mengine ajali hiyo ilipotokea saa moja usiku mnamo Jumatatu.
Bw Onyango alisema basi lilijaribu kurudi kwa upande wake barabarani lakini lori la trela likaligonga ubavuni.
“Hatukuwa tumeona basi likiyumba kimitambo kabla ya kutokea kwa ajali,”akasema Bw Onyango.
Gavana wa Taita Taveta na Naibu Gavana Christine Kilalo waliwatembelea manusura wa ajali ambapo alisema kaunti inafuta bili za walioumia.
Gavana Mwadime aliahidi kwamba serikali ya kaunti ina mpango wa kujenga kituo spesheli kushughulikia wagonjwa wa ajali kwa sababu ajali nyingi hutokea katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.
“Tunafanya mazungumzo na washirika wetu wa maendeleo kuimarisha huduma, miundomsingi na vifaa katika hii hospitali,”akasema Bw Mwadime.
Aliongeza kwamba mradi huo utatimizwa kwa sababu ya idadi kubwa ya ajali zinazotokea na ulazima wa majeruhi kupelekwa katika hospitali ya Moi mjini Voi.