‘Alisema ameweka mitego Ikulu, yuko wapi sasa?’ Raila akejeli Gachagua akiwa hafla Vihiga
WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga ameonekana kurejelea siasa za nchini baada ya kumchekelea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua akisema masaibu yanayomzonga ni ya kujitakia.
Bw Odinga, anayewania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Mataifa (AUC) Jumapili, Disemba 1, 2024 alidai kuwa kutimuliwa kwa Bw Gachagua na shambulio dhidi yake katika hafla moja ya mazishi Limuru, Kiambu, Alhamisi wiki jana “ni shida ambazo Gachagua alijiletea mwenyewe.”
Akitumia lugha ya mafumbo na vitendawili (ilivyo kawaida yake), kiongozi huyo wa ODM alisema “mitego” ambayo Gachagua aliwekea serikali kumzuia kushirikiana na Rais William Ruto imeishia kumnasa yeye mwenyewe.
Bw Odinga alisema kuwa licha ya naibu huyo wa rais wa zamani kujigamba kuwa ameziba mianya ambayo huenda ikamwezesha yeye (Raila) kuingia katika Ikulu, Gachagua ndio ametimuliwa serikalini.
Handisheki au nusu mkate
“Alisema hakutakuwa na handisheki au serikali ya nusu mkate. Alijigamba kuwa ameweka mitego katika milango yote yote ya kuingia Ikulu. Wapi yeye sasa?” Bw Odinga akauliza.
Kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya alisema hayo jana katika uwanja wa Shule ya Upili ya Chavakali katika Kaunti ya Vihiga wakati wa hafla ya kutoa shukrani kufuatia kuteuliwa kwa Seneta wa kaunti hiyo Godfrey Ososti kuwa mmoja wa manaibu watatu wa kiongozi wa ODM.
Bw Osotsi alitunukiwa wadhifa huo baada ya kujaza nafasi ya gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya aliyejiuzulu wadhifa kufuatia uteuzi wake kuwa Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika.
Manaibu wengine wa kiongozi wa ODM ni Gavana wa Kisii Simba Arati na mwenzake wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir.
Bw Nassir alitunukiwa wadhifa huo kufuatia kujiuzulu kwa mtangulizi wake Ali Hassan Joho aliyeteuliwa na Rais Ruto kuwa Waziri wa Uchimbaji Madini na Uchumi wa Majini.
Mabw Joho na Oparanya, ambao walikuwa manaibu wa kiongozi wa ODM, pamoja na aliyekuwa mwenyeketi wa chama hicho John Mbadi, aliyekuwa kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi ya chama hicho cha Chungwa Beatrice Askul ndio walioteuliwa na Rais Ruto katika baraza la mawaziri kufuatia kufufuliwa kwa ukuruba kati yake na Bw Odinga.
Ukuruba na Ruto
Ukuruba huo ulijiri baada machafuko yaliyosababishwa maandamano ya vijana wa kizazi cha sasa Gen Zs wakipinga Mswada wa Fedha wa 2024 na utawala mbaya wa serikali hii.
Kilele cha msururu wa maandamano hayo kilikuwa uvamizi wa majengo ya Bunge mnamo Juni 25, 2024, dakika chache baada ya wabunge kuupitisha mswada huo uliopendekeza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa na huduma za kimsingi.
Baada ya Rais Ruto kushinda uchaguzi urais wa 2022, Bw Gachagua, wakati huo akiwa naibu rais, alitangaza kuwa ameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Bw Odinga hapenyezi na kuingia katika serikali ya Kenya Kwanza kupitia mlango wa nyuma.
Hata hivyo, karibu miaka miwili baadaye, uhusiano kati yake na bosi wake (Rais Ruto) ulianza kudorora. Bw Gachagua, ambaye ni Mbunge wa Mathira, alianza kukosa na wandani wa Rais Ruto huku akionekana kupinga baadhi ya maamuzi ya baraza la mawaziri na serikali aliyokuwa akiihudumia.
Hatimaye, alitumuliwa afisini baada ya hoja iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse kupitishwa katika Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 8, 2024 na kupitishwa katika Seneti mnamo Oktoba 17, 2024.
Kindiki aliapishwa
Baada ya juhudi zake za kuzuia wadhifa huo kupewa mtu mwingine kugonga mwamba kortini mnamo Novemba 1, 2024, Profesa Kithure Kindiki aliapishwa rasmi kuwa Naibu Rais wa tatu chini ya katiba hii.
Jana, Bw Odinga aliweka wazi kuwa japo sasa anaelekeza juhudi zake katika kampeni za uenyekiti wa AUC, hatachelea kutoa kauli zake kuhusiana na siasa za humu nchini.
Wakati huo, Bw Odinga na viongozi wakuu wa ODM, walioandamana naye walikariri kuwa chama hicho kitadhamini mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Tangazo hilo linaonekana kutia walakini kuhusu dhana kwamba chama hicho kinapania kubuni muungano na kile cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto kwa lengo la kumuunga mkono rais huyo atakapokuwa akitetea kiti chake 2027.