• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Aliyekuwa Naibu Kamishna ashangaa kugeuzwa ‘mahabusu’ kwa ulaghai wa shamba la mabilioni  

Aliyekuwa Naibu Kamishna ashangaa kugeuzwa ‘mahabusu’ kwa ulaghai wa shamba la mabilioni  

NA RICHARD MUNGUTI

KUSIKIZWA kwa kesi ya ulaghai wa shamba la Sh1.35 bilioni dhidi ya aliyekuwa Naibu Kamishna wa Nairobi, Davis Nathan Chelogoi Jumanne, Aprili 9, 2024 kulikumbwa na hitilafu upande wa mashtaka ulipowasilisha ushahidi mpya dhidi yake dakika ya mwisho.

Kuwasilishwa kwa hati 29 mpya za umiliki wa shamba hilo kulimduwaza Bw Chelogoi hata ikabidi hakimu mwandamizi Dolphina Alego kumshtumu afisa anayechunguza kesi hiyo “kwa kumkabidhi mshtakiwa ushahidi mpya dakika ya mwisho.”

Wakili Brian Asa anayemtetea Chelogoi aliteta kwamba “kesi hiyo inaendelezwa kwa njia ya kuviziana”.

Bw Asa alisema alikabidhiwa ushahidi mpya wa hatimiliki 29 na afisa anayechunguza kesi hiyo Ijumaa, Aprili 5, 2024 na hakuwa na wakati wa “kufika katika afisi za ardhi kuzithibitisha.”

Kufuatia tukio hilo, wakili aliomba kesi hiyo itengewe siku nyingine ya kusikizwa ili apate maelezo zaidi kutoka kwa Chelogoi.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 29,2024 ambapo itaanza kusikizwa.

Bi Alego alimzomea mchunguzi wa kesi hiyo akisema “muda wa kumkabidhi mshtakiwa nakala za mashtaka na ushahidi ulikuwa umeyoyoma na kamwe hataruhusu ushahidi kuendelea kusukumiwa mshtakiwa bila mpango.”

Chelogoi ameshtakiwa kwa kumlaghai Ashok Shah na Hitenkumar Raja shamba lenye ukubwa wa ekari 18 eneo la Lower Kabete la thamani ya Sh1.35 bilioni.

Mshtakiwa amekana mashtaka manane ya kughushi stakabadhi za hatimiliki za shamba hilo.

Yuko nje kwa dhamana ya Sh2.5 milioni.

Chelogoi alishtakiwa Machi 21, 2024 baada ya kuhepa kufika kortini mara tano tangu Desemba 22, 2023.

Bw Chelogoi alifika kortini kufuatia ilani ya kumkamata kutolewa na Bi Alego.

Hakimu alikuwa ameamuru wasimamizi wa Nairobi Hospital wamfikishe kortini Bw Chelogoi kujibu mashtaka manane ya ulaghai wa shamba lenye utata ambalo wamiliki wake halisi ni Ashok Rupshi Shah na Hitenkumar Amritlal Raja.

“Nilikuwa nimemweleza mshtakiwa anatakiwa kufika kortini Machi 22, 2024 kujibu mashtaka,” Wakili Prof Tom Ojienda anayemwakilisha Bw Chelogoi pamoja na Bw Asa alimweleza hakimu.

Prof Ojienda alieleza mahakama mshtakiwa amekuwa mgonjwa na kwamba “amekuwa akilazwa Nairobi Hospital”.

Wakili huyo alisema Desemba 22, 2023 kibali cha kumtia nguvuni kilipotolewa, Bw Chelogoi alikuwa nchini Uganda.

Hata hivyo, hakimu aliamuru mshtakiwa asomewe mashtaka dhidi yake kisha Prof Ojienda akaomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu “ikitiliwa maanani alihudumia serikali miaka 40 kabla ya kustaafu 2020”.

Kiongozi wa mashtaka Bi Sonnia Njoki na wakili Suleiman Bashir anayewawakilisha Ashok na Raja walipinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana wakisema “ni tisho kwa walalamishi na atatoroka”.

Bi Njoki alieleza mahakama mshtakiwa amehepa kufika kortini mara tano na “kila kesi hiyo inapotajwa kunatolewa sababu zake kutofika kortini kujibu mashtaka”.

Korti ilielezwa na Bw Bashir kwamba “mahakama inapaswa kumsukuma mshtakiwa gerezani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa”.

Hakimu aliombwa atilie maanani tabia ya mshtakiwa ya kuhepa kufika kortini.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka dhidi yake.

Bi Alego aliamuru mshtakiwa asukumwe gereza la viwandani hadi Machi 25, 2024 atakapofikishwa kortini tena mahakama itoe uamuzi endapo itamwachilia kwa dhamana au la.

“Kwa sasa mshtakiwa atapelekwa rumande hadi Machi 25, 2024 nitakapoamua kuhusu ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana,” Bi Alego alisema.

Hakimu alisema baada ya mshtakiwa kujibu mashtaka hali yake hubadilika na huwa mahabusu chini ya ulinzi wa idara ya magereza.

“Agizo hilo lina maana kwamba mimi ni mahabusu. Nitaenda korokoro ya Idara ya Magereza?” Bw Chelogoi alimwuliza Prof Ojienda.

Jaribio la Prof Ojienda kuomba mshtakiwa arudishwe Nairobi Hospital liligonga mwamba, hakimu alipomweleza hali ya mshtakiwa imebadilika baada ya kujibu mashtaka.

“Sitaki kujadili mno suala hili la kule atakakopelekwa mshtakiwa baada ya kujibu shtaka. Nataka kusoma na kutathmini mawasilisho yenu ili nitoe uamuzi kuhusu ombi la dhamana,” Bi Alego alisema huku akiamuru mshtakiwa ashughulikiwe na idara ya magereza.

Bw Chelogoi ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi katika Idara ya Mipango ya Wizara ya Ardhi, Bw Andrew Aseri Kirungu.

Wawili hao; Chelogoi na Kirungu wanakabiliwa na shtaka la kula njama kulaghai Ashok Rupshi Shah na Hitenkumar Amritlal Raja lao.

Bw Chelogoi anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na unyakuzi wa shamba hilo.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Kisii yaruhusiwa kukusanya ushuru Keroka

Mwindaji ageuka mwindwa: Afisa wa DCI akamatwa akiitisha...

T L