Aliyekuwa waziri Cyrus Jirongo afariki kwenye ajali
Aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, ameaga dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mapema Jumamosi usiku katika barabara kuu ya Nakuru–Naivasha.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi kutoka Kituo cha Naivasha, ajali hiyo ilitokea leo, Desemba 13, 2025, saa tisa usiku katika eneo la Karai. Jirongo, mwenye umri wa miaka 64, alikuwa akiendesha gari aina ya Mercedes Benz lenye nambari ya usajili KCZ 305C kutoka upande wa Nakuru akielekea Nairobi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa alipofika eneo la ajali, alishindwa kudhibiti gari lake na likatoka laini yake sahihi, hali iliyosababisha kugongana ana kwa ana na basi lenye nambari ya usajili KCU 576A, linalomilikiwa na kampuni ya Climax. Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Tiras Kamau Githinji, mwenye umri wa miaka 52, ambaye alikuwa akitokea upande wa Nairobi akielekea Nakuru.
Kutokana na ajali hiyo, Jirongo alipata majeraha makubwa ya kichwa na alifariki papo hapo. Polisi walifika eneo la tukio na kuchukua hatua zinazohitajika. Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.
Magari yote mawili yalivutwa hadi kituo cha polisi na kuzuiliwa kwa uchunguzi zaidi wa kiufundi. Polisi wamesema chanzo cha ajali bado kinachunguzwa,
Jirongo aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Maendeleo ya Maeneo ya Mashambani katika utawala wa hayati Rais Daniel Moi mwaka 2002, na pia alikuwa Mbunge wa Lugari katika mihula miwili tofauti.
Kifo chake kimezua huzuni miongoni mwa viongozi na wananchi, wengi wakimtaja kama mwanasiasa na mfanyabiashara aliyetoa mchango mkubwa katika siasa za Kenya.