Habari za Kitaifa

Amerika haikulipia ndege ya kifahari iliyombeba Ruto, msemaji wa ubalozi afafanua

May 21st, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Amerika haikulipia ndege ya kibinafsi ya kifahari aliyotumia Rais William Ruto kusafiria kwenda Amerika, msemaji wa Ubalozi wa Amerika nchini Kenya amesema.

Kulikuwa na habari za kukanganya iwapo ndege ya kifahari aliyotumia kiongozi wa nchi ilikuwa imelipiwa na Amerika au Mkenya mlipa ushuru.

Ziara ya Kiserikali ya siku nne anayoendelea nayo nchini humo kwa kawaida humaanisha kwamba gharama zote zimeshughulikiwa na taifa lililotoa mwaliko, kwa maana hii, basi iliaminika kwamba Amerika ndio imegharamia usafiri.

Lakini sasa tamko la msemaji wa Ubalozi wa Amerika linamaanisha kwamba Wakenya wamekohoa Sh71 milioni kwenda pekee, wakati ambapo wengi wanalia kuhusu ushuru wa juu na gharama ya maisha nchini.

“Nataka kuweka wazi, Serikali ya Amerika haikulipia ndege ya kibinafsi aliyotumia Rais Ruto,” akanukuliwa balozi huyo akisema.

Kwa kawaida, kiongozi wa nchi hutumia ndege za Jeshi kwa ziara yake lakini katika ziara hii, Rais aliamua kutumia ndege ya kifahari ya kibinafsi.