Habari za Kitaifa

Amerika yakataza raia wake kuanikia wezi mapambo ya thamani

March 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KEVIN CHERUIYOT Na CHARLES WASONGA

AMERIKA imewataka raia wake nchini kuwa waangalifu kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu vinavyoshuhudiwa katika mitaa ya makazi jijini Nairobi.

Kwenye taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya ubalozi wake nchini Kenya mnamo Ijumaa, taifa hilo linawaonya raia wake na kuwataka kuficha mali yao ya thamani kama vile saa, simu, mikufu na aina nyingine ya ‘bling bling’ wanapotembea katika mitaa ya Nairobi.

“Kuna ripoti ya ongezeko la uhalifu katika mitaa ya makazi jijini Nairobi. Visa hivyo, vinajumuisha upokonyaji wa vibeti na simu. Serikali ya Kenya inachukua hatua ya kuongeza idadi ya polisi katika maeneo ambako uhalifu umekithiri,” ikasema taarifa hiyo.

Raia wa Amerika wameshauriwa kuwa waangalifu na wakome “kuonyesha dalili za utajiri wao, kama vile kuvalia vipuli ghali au saa au kuweka wazi kiasi kikubwa cha pesa”.

Aidha, ubalozi wa Amerika umewashauri raia wake kuhakikisha milango ya magari yao imefungwa na vioo vya madirisha vimepandishwa juu wakiwa ndani magari yao hayo.

“Aidha, raia Waamerika wanashauriwa kujiepusha na maeneo yenye makabiliano au penye uwezekano wa kuwepo wahalifu,” taarifa ikaeleza.

Mwaka 2023, Waziri wa Usalama Kithure Kindiki alisema uhalifu mijini, ambao ni tishio kwa usalama wa wakazi na wafanyabiashara, ulikuwa umedhibitiwa.

Wakati huo, visa vingi vilikuwa vikiripotiwa ambapo makundi ya wahalifu wenye visu na silaha nyingine hatari walikuwa wakitishia maisha ya wakazi.

“Uongozi na wakuu wa polisi wamebadili doria za polisi jijini Nairobi mara moja. Aidha, Huduma ya Kitaifa ya Polisi imewatuma maafisa kutoka vikosi mbalimbali katika barabara za jiji kwa lengo la kuwakamata wahalifu hao na kuwapelea mahala wananakostahili kukaa,” Prof Kindiki akaeleza.