Habari za Kitaifa

Amerika yaanika ‘uozo uliokolea Kenya’ wa mauaji, dhuluma na uvunjaji wa sheria

Na DANIEL OGETTA, MERCY SIMIYU August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

AMERIKA imekemea Kenya kwa dhuluma, mauaji na uvunjaji wa sheria, ikisema kuwa kuzingatiwa kwa haki za kibinadamu kulidorora hasa wakati wa maandamano ya Gen Z Juni na Julai 2024.

Kupitia ripoti ambayo ilitolewa na nchi hiyo, ni kipindi hicho ambapo maafisa wa usalama walilaumiwa kwa mauaji ya kiholela, dhuluma, kamatakamata za kiholela na kuwazuilia waandamanaji kupigania haki zao.

Ingawa serikali ilichukua hatua kuwatambua na kuwaadhibu waliovunja sheria, kulikuwa na mapuuza na ukiukaji mkubwa wa sheria kwenye viwango vyote vya serikali, ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo yenye mada ‘Ukiukaji wa Haki za Kibinadamu 2024’ imelaumu serikali kwa kufeli kuhakikisha kuwa polisi waliovunja sheria wakati wa maandamano ya Gen Z Juni na Julai mwaka jana, wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Polisi wakati huo walikataa kuchunguzwa na wakawazuilia baadhi ya wanaharakati ambao walikuwa wamelalamika kuhusu kudhulumiwa,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.

“Badala ya kuwaadhibu polisi ambao walikuwa wamehusika, waliwahamisha polisi hao na kutumia ujanja kuhakikisha wengine hawawajibikii vitendo vyao,” ikaongeza ripoti hiyo.

Kuhusu mauaji ya kiholela, ripoti hiyo inasema kulikuwa na visa vingi vya mauaji yaliyotekelezwa na maafisa wa usalama wakati wa maandamano ya kupinga kuongezwa kwa ushuru kwenye Mswada wa Fedha 2024.