• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Anti-femicide: Kula ‘fare’ kusipandishe hasira, wanaume washauriwa

Anti-femicide: Kula ‘fare’ kusipandishe hasira, wanaume washauriwa

NA TITUS OMINDE

WANAUME wameambiwa wasiwaue wanawake wanaokula ‘fare’ na badala yake wakumbatie changamoto hiyo kama kichocheo kwao kuongeza ladha katika mistari yao ya kuwabembeleza kuingia boksi.

‘Fare’ ni neno lililokita mizizi nchini na mbali na pesa za nauli ambazo wanaume huwatumia wapenzi wao wa kike, pia hujumuisha pesa za matumizi kwa wanawake.

Lakini kwa muda mrefu wanaume wamekuwa wakilia kwamba baadhi ya wanawake hula ‘fare’ na kukataa kuwatembelea jinsi wanavyokuwa wamekubaliana.

Mnamo Jumamosi wakati wa maandamano ya kupinga mauaji yanayowalenga wanawake, wanaume waliambiwa wasiwe wepesi wa kupanda hasira endapo watakuwa waathiriwa wa wanawake kula fare.

Baadhi ya wanaume waliojiunga na maandamano hayo yaliyopewa jina la ‘Feminists March Against Femicide’ mjini Eldoret, waliwasihi wanaume kutowaua wanawake wanaokula nauli na badala yake watumie mbinu za kidiplomasia, kimaadili na hata kisheria kusuluhisha mgogoro.

“Kula nauli na fedha nyingine wanaume wanawatumia wanawake wanaochumbiana nao si kibali cha kuwatoa uhai na kuhalalisha mwelekeo unaoibuka wa wanawake kuuawa kiholela nchini. Mwanamume anafaa kuwa mtu jasiri anayetumia changamoto ya aina hiyo kama fursa ya kuibuka na mikakati mizuri,” akashauri Bw David Lelei kutoka mtandao wa Mashirika ya Kijamii Uasin Gishu.

Maoni yake yaliungwa mkono na kiongozi wa vijana wa Uasin Gishu Ben Kibet, ambaye aliwataka vijana wa kiume kukoma kuwaua wanawake.

Bw Kibet aliwataka wabunge kutunga sheria ambazo zitasaidia katika kupunguza visa vya mauaji ya wanawake nchini.

Mnamo 2023 mahakama ya madai madogo ya Eldoret ilitangaza kuwa haikuwa na mamlaka ya kusimamia kesi za wanawake kula nauli.

Soma Pia: Mwanamume abubujikwa na machozi demu kula nauli aliyomfulizia kuipata

Wakati wa maandamano yaliyoongozwa na wanariadha wa kimataifa kutoka taasisi ya Agnes Tirop Angels, wanariadha wa kike wakiongozwa na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Viola Lagat, walisikitika kwamba wanariadha wa kike ni miongoni mwa waathiriwa wakuu wa mauaji ya aina hiyo.

“Tulimpoteza mwanariadha Agnes Tirop kwa njia hiyo ya kikatili. Tukio hilo lingali linanisumbua sana. Tunatakiwa kusimama pamoja na kufanya kila tuwezalo kukomesha matukio hayo. Haikubaliki kumuua mtu kwa sababu tu amekataa kuwa kwa uhusiano wa kimapenzi nawe,” akasema Bi Lagat.

Wanaharakati wanaotetea haki za wanawake kutoka eneo la North Rift walitumia maandamano hayo kutaka bunge kutunga sheria zitakazowalinda wanawake dhidi ya visa vinavyoongezeka vya mauaji yanayowalenga nchini.

“Kila kitu kinapaswa kufanywa kwa njia zote ili kuwazuia wanaume kuwaua wanawake, tunahitaji kubuni sheria ya kuwaadhibu zaidi wanaume wanaowaua wanawake kutokana na tofauti za kimahusiano,” alisema Bi Mercy Chepkurui ambaye ni mwanaharakati wa haki za wanawake kutoka Uasin Gishu.

Bi Chepkurui anataka serikali itangaze mauaji yanayowalenga wanawake kuwa janga la kitaifa na pia kupitia upya kanuni za adhabu ili kurejesha hukumu ya kifo kwa wanaume ambao watapatikana na hatia ya mauaji ya wanawake.

“Hukumu ya kifo na kifungo cha maisha jela vinafaa kuwa adhabu inayofaa na serikali inapaswa kutangaza mauaji ya wanawake kuwa janga la kitaifa,” alisema Bi Chepkurui.

Bi Mariamu Suleiman kutoka kituo cha Centre Against Torture ni mmojawapo wa waandamanaji waliojitokeza kupinga mauaji dhidi ya wanawake mjini Eldoret mnamo Januari 27, 2024. PICHA | TITUS OMINDE

Wafanyabiashara ya ngono kutoka Eldoret ambao pia walishiriki maandamano hayo walifichua kwamba nyakati fulani wamepoteza wenzao kupitia mauaji ya aina hiyo.

Baadhi waliozungumza na Taifa Jumapili kwa masharti kwamba wasitajwe, walisema ikizingatiwa kuwa biashara yao inachukuliwa ni haramu nchini, imekuwa vigumu kwao kutafuta haki kwa wenzao ambao ni waathiriwa wa mauaji.

“Kwa muda mrefu wenzetu wamekuwa waathiriwa wa mauaji lakini tunapata ugumu kujitokeza na kupigania haki zao kwani biashara yetu inachukuliwa kuwa haramu katika nchi yetu,” mmoja wa wafanyabiashara ya ngono mjini Eldoret alisema.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa sita wakamatwa kwa kuteketeza bangi, kusaidia...

Serikali yasambaza mbolea kwa tahadhari kuu

T L