Arati achemsha Eldoret, amtaka Ruto aachane na UDA arejee ODM
NAIBU Kiongozi wa ODM Simba Arati Jumatatu, Desemba 15, 2025 alisema Rais William Ruto amekaribishwa kujiunga tena na chama hicho huku akiahidi kwamba wataendelea kushirikiana naye katika Serikali Jumuishi.
Bw Arati aliongoza mkutano mkubwa wa ODM katikati mwa jiji la Eldoret ambapo alisema chama hicho kina mizizi yake kote nchini.
Kiongozi huyo alimtaka Rais Ruto agure UDA na kurejea ODM hatua aliyosema itasaidia Serikali Jumuishi kuendelea kuwa dhabiti jinsi alivyotaka aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.
“Leo niko hapa Eldoret ngome ya kisiasa ya Rais William Ruto kuonyesha kuwa ODM ni chama cha kitaifa. Tunaunga mkono Serikali Jumuishi alivyotuacha Raila Odinga kwa sababu umoja wetu ni udhabiti wetu,” akasema Bw Arati.
Gavana huyo wa Kisii alisema kuwa ODM haitaendelea kuwa upinzani kwenye serikali inayokuja na lazima iingie serikalini.
“Serikali Jumuishi inaendelea kupiga hatua na nina hakika kuwa kivyovyote vile ODM itakuwa serikali baada ya 2027,” akasisitiza.
Bw Arati alionekana kushajishwa na mapokezi ambayo alipata katika ngome hiyo ya UDA.
Ili kupiga jeki hoja yake, alimtaka Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii kuyajumuisha makabila yote ndani ya serikali yake.
Pia alimwomba gavana huyo akome kuwahangaisha wafanyabiashara wadogo wadogo.
“Naomba kaunti iwape ajira Wakenya kutoka makabila yote na awaruhusu wafanyabiashara na wahudumu wa bodaboda bila kusumbuliwa hasa msimu huu wa sherehe,” akasema.
Jana jiji hilo lilijaa rangi ya chungwa kufuatia ziara hiyo, tukio ambalo linaweza kulinganishwa tu na mnamo 2007 wakati Rais Ruto na Bw Odinga walikuwa kambi moja kisiasa.
Awali kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga walimtembelea Gavana Bii ambao walisisitiza kuwa watafanya kazi na Rais hadi 2027 kabla ya kutoa mwelekeo zaidi.