Arati motoni kwa kukiuka agizo la Waziri Machogu
Na RUTH MBULA
GAVANA wa Kisii, Simba Arati amekiuka agizo la waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na kuendelea kusambaza mifuko ya shule iliyo na picha yake kwa mamia ya wanafunzi katika kaunti hiyo.
Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu alipiga marufuku uwekaji picha za mwanasiasa katika nyenzo za masomo wanazogawia wanafunzi.
Bw Arati anasema hakuna kitakachomzuia kutoa mifuko iliyo na jina na picha yake, huku baadhi ya maafisa wake wakitishia kufika kortini kupinga marufuku ya Machogu, ambayo walidai haina msingi wa kisheria.
Bw Arati anatoa mifuko hiyo kwa wanafunzi wanaosoma katika kaunti nzima, kupitia mpango wake wa “Elimu na Simba”’.
Mpango huo unafadhiliwa kibinafsi na ulianza punde tu baada ya Arati kuwa Gavana wa Kisii, kwa kile alichosema kililenga kusaidia watoto werevu kutoka familia maskini walio na kiu ya kupata elimu.
“Mifuko hiyo hainunuliwi kwa kutumia fedha za kaunti. Pia tunasambaza mifuko hiyo vijijini na sio maeneo ya shule. Hakuna aliye na sababu ya kutuzuia,” Bw Arati akasema.
Gavana Arati alisema hataheshimu agizo la Waziri wa Elimu, na ataendelea kuwapa watoto mifuko hiyo kote katika kaunti hiyo.
Wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka mpya katika wadi ya Ibeno eneo bunge la Nyaribari Chache, Bw Arati aliwapa watoto zaidi ya 2000 mifuko ya shule.