Arati, Nassir waashiria Raila ana risasi ya kufyatua 2027
HUENDA jina la Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga likawa kwenye debe kama mgombea urais katika uchaguzi wa 2027, ikiwa kauli za viongozi wapya wa chama cha ODM zitatimia.
Kundi la wanasiasa kutoka chama hicho limemwidhinisha waziri mkuu huyo wa zamani kuwa mgombeaji wanayempendelea kumtimua Rais William Ruto kutoka ikuluni.
Naibu viongozi wa chama cha ODM Simba Arati na Abdullswamad Nassir walisema wanamuunga kiongozi wa chama chao katika shughuli zake za kisiasa nchini.
Bw Odinga kwa sasa analenga uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.
Lakini pia anashiriki katika siasa za humu nchini, hasa jinsi nchi inatawaliwa na serikali ya Kenya Kwanza.
Viongozi wakuu wa ODM walisema watamuunga kinara huyo wa upinzani katika mwelekeo wowote wa kisiasa atakaochukua.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kisiasa Jumamosi ulioandaliwa na Mbunge wa Kasipul, Bw Ong’ondo Were katika Mji wa Oyugis, Bw Arati alisema licha ya waziri mkuu huyo wa zamani kugombea wadhifa wa bara, hapaswi kusahau nchi yake.
“Tunaunga mkono azma ya Baba (Bw Odinga) kuwa kiongozi wa AU. Lakini asiifumbie macho nchi baada ya kufika huko,” gavana huyo wa Kisii alisema.
Kulingana na Bw Arati, kiongozi wa chama chao bado anaweza kuwania urais katika uchaguzi ujao.
Alidai hilo linawezekana hata ikiwa Bw Odinga atashinda wadhifa wa AU.
“Baba anaweza kurejea nchini miezi michache kabla ya uchaguzi kuwania urais. Tutahakikisha tunashindana na William Ruto,” Bw Arati alisema.
Kauli ya Bw Arati ilinuiwa kuwazuia wanasiasa wengine ambao wanamezea mate urais kwa tiketi ya Azimio.
Ndani ya muungano wa Azimio, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametangaza kuwa atashindana na Dkt Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Hata hivyo, Bw Arati alisema kuwa chama cha ODM hakitamwacha mtu mwingine kuchukua nafasi ambayo wamemtengea waziri mkuu huyo wa zamani.
Litakuwa jaribio la sita kwa Bw Odinga kuwa rais wa Kenya iwapo atagombea wadhifa huo katika uchaguzi mkuu ujao.
Japo anamezea mate uenyekiti wa AU, Bw Odinga amekuwa makini na siasa nchini huku washirika wake sita wakiteuliwa mawaziri.
Gavana Arati aliwahakikishia wafuasi wa ODM kwamba Bw Odinga ndiye anayesimamia upinzani na ataendelea kuikosoa serikali.
Ingawa waziri mkuu huyo wa zamani alikubali kufanya kazi na rais, gavana huyo alieleza kuwa haimaanishi kuwa ODM imejiunga na serikali ya Kenya Kwanza.