• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Asenath Cheruto: Tulikuwa tufunge harusi kubwa na Kiptum Aprili

Asenath Cheruto: Tulikuwa tufunge harusi kubwa na Kiptum Aprili

CAROLINE WAFULA NA FRIDAH OKACHI

MWANARIADHA Kelvin Kiptum alikuwa akipanga harusi ya kupendeza ili kurasimisha ndoa yake na mkewe Asenath Cheruto mwaka huu.

Asenath, ambaye sasa amesalia kuwa mjane, amefichua walikuwa kwenye harakati za kufunga ndoa. Mwanariadha huyo na mkewe walikuwa wamepanga kufanya harusi ya kupendeza mnamo Aprili, 2024.

Mwezi huu marehemu ambaye ni bingwa wa marathon, alikuwa akienda kukimbia katika Marathon ya Rotterdam mnamo Aprili 14.

Bi Cheruto aliyejawa na majonzi, akiandamana na watoto wao wawili Caleb, 7, na Precious, 4, aliomboleza marehemu mumewe kama mwanamume mwenye upendo na kujali ambaye aliithamini sana familia yake.

Aliambia umati uliohudhuria hafla ya mazishi ya mwanariadha huyo katika uwanja wa Chepkorio eneo bunge la Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet kwamba angeendelea na kuweka viapo vyake vya mapenzi hata asipokuwepo.

“Bado nitafanya ahadi zangu za upendo hata wakati haupo,” alisema Bi Cheruto akiwa na wingi wa majonzi.

Rais William Ruto, Naibu wake Rigathi Gachagua, wanariadha wakuu na maafisa wa riadha ni miongoni mwa watu mashuhuri wanaohudhuria hafla ya mazishi. Marehemu Kiptum alioana na Bi Cheruto mwaka wa 2017 katika sherehe ya kitamaduni, hii ni kulingana na wasifu uliochapishwa.

Bi Cheruto alijuta kwamba hawakuweza kufurahia matunda ya kazi ya mumewe kama familia changa, na kuahidi kusalia imara kwa watoto wao wawili, na kwa heshima yake. Marehemu Kiptum alikuwa mtoto wa pekee wa babake Samson Cheruiyoit na mama Mary Kangogo na alikuwa na dada wa kambo-Rhodah Chemutai

“Nakuomboleza mpenzi wangu na ninaahidi kuwa imara kwa ajili ya watoto wetu. Ninaahidi kuwafanya watabasamu kwa heshima yako, naahidi kukufurahisha,” aliongeza Bi Cheruto.

Waombolezaji walijitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho kwa mwanariadha huyo, aliyesherehekewa kimataifa.

Rais wa riadha nchini Jackson Tuwei alimwomba Gavana Kiptum Wisley Rotich kumwajiri mjane huyo katika Serikali ya Kaunti ya Elgeyo Marakwet ili awe karibu na nyumbani na aweze kutunza familia.

Bw Kiptum amezikwa katika nyumba yake mpya katika shamba lake la Cherunya huko Naiberi, Kaunti ya Uasin Gishu, Ijumaa, Februari 23.

Mwili wake ulilala nyumbani kwake Chepsamo Alhamisi usiku kabla ya mazishi.

Mapema Alhamisi kulikuwa na msafara wa mazishi kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Eldoret hadi Iten, ili kutazamwa na umma, kabla ya kumalizia nyumbani kwake Chepsamo.

  • Tags

You can share this post!

Askofu David ‘Gakuyo’ Ngari kuzuiliwa hadi...

Wakulima Taita Taveta kujinyanyua na mbolea nafuu, upimaji...

T L