• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Askofu David ‘Gakuyo’ Ngari kuzuiliwa hadi Jumatatu kesi ya kupora Sh1bn

Askofu David ‘Gakuyo’ Ngari kuzuiliwa hadi Jumatatu kesi ya kupora Sh1bn

NA RICHARD MUNGUTI

ASKOFU anayedaiwa kuwapora Wakenya 50,000 zaidi ya Sh1 bilioni akidai ni kuwekeza katika biashara ya ujenzi wa nyumba, atazuiliwa na polisi hadi Jumatatu atakaposhtakiwa.

Hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo aliamuru Askofu David Kariuki Ngari almaarufu Gakuyo wa Kanisa la Chosen Calvary azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga wachunguzi wakamilishe kuandika taarifa za mashahidi.

Akiamuru Askofu Ngari awekwe rumande, Bw Onsarigo alisema kesi inayomkabili mhubiri huyo “iko na umuhimu mkubwa kwa umma.”

Hakimu alisema lazima polisi wapewe muda wa kukamilisha mahojiano na kuandikisha taarifa za mashahidi.

“Kesi hii inawahusu watu zaidi 50,000 wanaodai walitapeliwa Sh1 bilioni na mhubiri huyu. Polisi wanahitaji muda kukamilisha uchunguzi ulioanza 2019 na ukayumbishwa na ugonjwa wa Covid-19 mwaka 2020,” akasema Bw Onsarigo.

Bi Teresia Munga ambaye ni mmojawapo wa waathiriwa, alitaka korti imweleze jinsi atakavyopata pesa zake Sh1 milioni alizodai alimpa Gakuyo.

Bi Teresia Munga (wa pili mbele kushoto) ambaye ni mmojawapo wa waathiriwa, alitaka korti imweleze jinsi atakavyopata pesa zake Sh1 milioni alizodai alimpa Askofu David Kariuki Ngari almaarufu Gakuyo. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Hakimu alisema Askofu Ngari alikamatwa akijaribu kutoroka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Embakasi, Nairobi mnamo Jumatano.

Gakuyo kama anavyofahamika na wengi alitiwa mbaroni na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga usiku wa Jumatano kabla ya kufikishwa kortini Alhamisi.

Akiomba pasta huyo–anayechunguzwa kwa makosa ya wizi, ulaghai na kula njama za kulaghai–azuiliwe kwa siku nne kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi wao, kiongozi wa mashtaka Henry Kinyanjui alisema “suala hili lina umuhimu wa umma.”

Mawakili wa Askofu Ngari–Danstan Omari, Mwenda Njagi, Shadrack Wambui, na Njiru Ndegwa–waliomba aachiliwe kwa dhamana, wakisema”uchunguzi umeendelea kwa miaka mitano na hajawahi kuvuruga utaratibu wa polisi kubaini ukweli.”

Mawakili hao waliwashutumu polisi kwa kumtia mbaroni askofu wakati mhubiri wa kimataifa Bennu Hinn anatua nchini kufanya krusedi kubwa katika uwanja wa Nyayo.

Pia Bw Omari alisema mhubiri huyo alikamatwa kwa shinikizo za wanasiasa wa Kaunti ya Kiambu aliopambana nao kuwania Ugavana wa kaunti hiyo.

Ndipo mahakama mnamo Ijumaa ikaamua askofu Ngari kuendelea kuzuiliwa badala ya kuachiliwa kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

Polisi watatu mashakani kwa kuitisha Sh200,000 kuwaachilia...

Asenath Cheruto: Tulikuwa tufunge harusi kubwa na Kiptum...

T L