• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Askofu Gakuyo kusalia rumande   

Askofu Gakuyo kusalia rumande  

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imempa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) muda wa mwezi mmoja aandae ushahidi katika kesi inayomkabili mhubiri matata Askofu David Kariuki Ngari almaarufu Gakuyo ya ulaghai wa Sh1.2 bilioni.

Hakimu mkazi Mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi aliamuru kesi ya Askofu Gakuyo itajwe tena Aprili 4, 2024 ili kuwezesha DPP kuandaa ushahidi dhidi ya mubiri huyo anayeshtakiwa kwa kulaghai watu 50, 000 zaidi ya Sh1 bilioni.

Bw Ekhubi alitoa agizo hilo kufuatia ombi la kiongozi wa mashtaka, Bi Alice Mathangani.

Bi Mathangani alimsihi Bw Ekhubi aruhusu afisi ya DPP iandae ushahidi wote kisha iwakabidhi mawakili wa Askofu Gakuyo.

“Kesi hii ilikuwa imeorodheshwa leo, Jumatatu, Machi 11, 2024, itengewe siku ya kusikizwa lakini afisi ya DPP haijawakabidhi mawakili wa mshtakiwa na nakala za mashahidi. Naomba muda wa mwezi mmoja kukamilisha zoezi hili,” Bi Mathangani alimweleza Bw Ekhubi.

Mahakama ilifahamishwa kwamba licha ya uchunguzi katika kesi hii kuanzishwa 2018 polisi hawajakamilisha kuandikisha taarifa za mashahidi wote.

Bi Mathangani aliomba muda zaidi kukamilisha zoezi hilo.

Alisema: “Ninatumaini katika muda wa mwezi mmoja, polisi watakuwa wamekamilisha zoezi la kuandikisha taarifa za mashahidi wote. Naomba kesi hii itajwe Aprili 4, 2024”.

Ombi hilo halikupingwa na mawakili wanaomtetea Askofu Gakuyo, akiwemo Daniel Wangenyi, Danstan Omari, Mwenda Njagi na Ndegwa Njiru.

“Hatupingi ombi hili la DPP kuomba muda zaidi,” Bw Wangenyi alimweleza hakimu.

Hakimu alikubalia ombi la DPP na kuamuru Askofu Gakuyo arudishwe rumande.

Askofu huyo ameshindwa kuweka dhamana ya Sh20 milioni kortini au kulipa dhamana ya pesa tasilimu Sh10 milioni.

Hakimu alikataa ombi la mshtakiwa kupunguziwa dhamana hiyo akisema “inalingana kiwango cha pesa anazodaiwa kuwafuja watu.”

 

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo: Nilishinikiza Kibaki kumteua Kenyatta kama Naibu...

Wapigeni risasi wanaoharibu miundo misingi- Kindiki

T L