Habari za Kitaifa

Askofu mstaafu wa jimbo la Kakamega la Kanisa Katoliki afariki dunia

November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Kanisa Katoliki nchini Kenya limepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu, Philip Sulumeti, mmoja wa viongozi wanaoheshimika zaidi katika historia ya Kanisa Katoliki nchini.

Taarifa kutoka Jimbo Katoliki la Kakamega zinasema kuwa Askofu Sulumeti alifariki dunia usiku wa Novemba 9, 2025, saa tano usiku, akiwa katika Hospitali ya Nairobi.

Akithibitisha taarifa hizo, Askofu wa sasa wa Kakamega, Joseph Obanyi, aliwataka waamini kuendelea kumuombea marehemu wakati mipango ya mazishi ikiandaliwa.
“Naomba tumkumbuke katika sala na misa zetu tunapoanza maandalizi ya mazishi yake. Taarifa kamili zitatolewa baadaye,” alisema Askofu Obanyi.
Aliwapa pole watu wote wa Mungu katika jimbo hilo, jamaa na marafiki wa marehemu, akiahidi maombi na faraja katika kipindi hiki kigumu.

Kifo cha Askofu Sulumeti kinamaliza safari ya kipekee ya karibu nusu karne ya utumishi wa Kanisa, uliogusa maisha ya kiroho, kijamii na kielimu katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

Alizaliwa Agosti 15 1937, na akatawazwa padre mnamo Januari 6, 1966 katika Jimbo Katoliki la Kisumu. Mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Kisumu na  akawa Askofu Agosti mwaka huo. Mnamo Desemba 1976 alirithi Askofu Joannes de Reeper kama Askofu wa Kisumu, kabla ya kuteuliwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Kakamega mnamo Februari 28, 1978.

Askofu Sulumeti alistaafu Desemba 5 2014, akiacha urithi mkubwa wa huduma, maendeleo na uaminifu kwa Kanisa Katoliki.